Wanawake washauriwa kuchangamkia mikopo

16Apr 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wanawake washauriwa kuchangamkia mikopo

WANAWAKE mkoani Mbeya wameshauriwa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ikiwamo mikopo ya halmashauri inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayotengwa kwa ajili ya kundi hilo.

Ushauri huo ulitolewa na Ofisa Biashara wa Wilaya ya Mbeya, Elizabeth Iyombe, alipokuwa anafunga mafunzo ya miezi mitatu ya ujasiriamali kwa zaidi ya wanawake wajasiriamali 100 wa Jiji la Mbeya ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali.

Mafunzo hayo yalikuwa yanatolewa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Mandela Washington Fellowship (MWF) kwa kushirikiana na ubalozi wa Marekani nchini, ambapo yalilenga kuwawezesha wanawake hao kuwa na uelewa juu ya njia za kufanya biashara zao kuwa endelevu.

Iyombe alisema kwa sasa kuna fursa nyingi za wanawake wajasiriamali hasa ambao tayari wamejiunga kwenye vikundi kwa madai kuwa kwa sasa kila anayetaka kuwasaidia anataka wawe kwenye vikundi.

Alisema pamoja na kwamba serikali imetenga asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya wanawake, lakini mwamko wa kundi hilo kujitokeza kukopa fedha hizo ni mdogo kutokana na kutojiunga na vikundi.

“Hongereni kwenu mliopata fursa ya kushiriki mafunzo haya naamini mtakuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha wenzenu kujiunga kwenye vikundi, halmashauri zetu zinatenga fedha kwa ajili yenu, lakini pia wapo wadau wanaojitolea kuwezesha vikundi,” alisema Iyombe.

Pia aliwataka kutumia vizuri elimu waliyoipata ili kuinua kipato cha familia zao na kuwa na uwezo wa kujitegemea katika maisha yao huku biashara zao zikiendelea kustawi.

Mratibu wa Mradi huo, Margret Simalenga, alisema mradi huo ulikuwa unawalenga zaidi wanawake ambao tayari wana biashara zao na kwamba yalilenga kuwapa mbinu za matumizi sahihi ya fedha za miradi yao.

Alisema miongoni mwa vitu ambavyo wajasiriamali hao wamefundishwa kwa siku hizo ilikuwa ni kuwa na madaftari ya kuandika vitu wanavyonunua na lingine kwa ajili ya kuandika vitu wanavyouza ili iwe rahisi kujua faida ya biashara zao.

Alisema walibaini kuwa baadhi ya wanawake wanaanzisha biashara ambazo zinakuwa sio endelevu kwa sababu wanashindwa kutofautisha fedha za biashara na fedha za matumizi ya nyumbani.

“Tilibaini kuwa baadhi ya biashara za wanawake zinakufa kwa sababu hawana tabia ya kuandika mapato na matumizi na hivyo wanajikuta wanachukua fedha za biashara wanazitumia kwenye matumizi mengine ya nyumbani na hivyo kuingia hasara,” alisema Simalenga.

Baadhi ya wajasiriamali waliohudhuria mafunzo hayo walisema yatawasaidia kubadili mwelekeo wa biashara zao kwa madai kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuwa na mtazamo tofauti.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Amina Mwambopo ambaye ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika Soko la Sokomatola jijini Mbeya, alisema mara nyingi wanawake wanashindwa kuendelea kwa sababu wanakuwa na tamaa ya kununua kila kitu.

Alisema wakati mwingine wanajikuta wanatumia fedha za biashara kwenye matumizi mengine ikiwamo kununua nguo na vyakula.

Vilevile wajasiriamali hao walishauriwa kurasimisha biashara zao kwa kuwa na leseni za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwa wale ambao mitaji yao bado midogo wanatakiwa wawe na vitaambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Rais.

Habari Kubwa