Wanawake wawezeshwa kushiriki kilimo

11Mar 2017
Raphael Kibiriti
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake wawezeshwa kushiriki kilimo

PROGRAMU ya Ubunifu katika Kilimo inayolenga kuwaongezea uwezo wakulima wadogo na hasa wanawake, imebainisha na kuendeleza zaidi ya ubunifu 30 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Land O’ Lakes nchini, Dk. Rose Kingamkono.

Kauli kuhusu hilo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Land O’ Lakes nchini, Dk. Rose Kingamkono, kwenye mkutano wa kuelezea utendaji wa shirika hilo, uliohusisha maofisa wa serikali.

Dk. Kingamkono alisema, Programu hiyo ilibainisha, kuendeleza na kutangaza jumla ya ubunifu 33 za kilimo kupitia Mradi wa Miaka Mitano wa Ubunifu Katika Usawa wa Kijinsia (IGE).

Mradi ambao ulifadhiliwa na Shirika la USAID la Marekani kwa kushirikiana na Kituo cha Kuendeleza Wanawake Katika Kilimo Tanzania (CAWAT), kuanzia mwaka 2012, ajili ya kuboresha usalama wa chakula katika ngazi ya kaya.

“Karibu asilimia 98 ya wanawake walioko vijijini wanajihusisha na kilimo nchini, ikitiliwa maanani kuwa asilimia 70 Watanzania wanaishi maeneo ya vijijini,” alisema na kuongeza:

“Wanawake hawa, ndiyo kundi kubwa linalochangia asilimia 52 ya nguvu kazi ya nchi hii, na hivyo kuwa uti wa mgongo kwa uchumi wa taifa.”

Dk. Kingamkono alisema, wanawake ndiyo kundi linalofanya sehemu kubwa ya kazi za kilimo kuanzia katika utayarishaji wa mashamba, kulima, palizi, uvunaji na uhifadhi wa mazao.

Habari Kubwa