Wanunuzi madini waiangukia serikali

29Jun 2022
Tumaini Mafie
Arusha
Nipashe
Wanunuzi madini waiangukia serikali

WANUNUZI wa madini nchini wameiomba serikali kufikiria kupunguza viwango vya ada ya leseni kutoka Sh. 250,000 kwa mwaka hadi kufikia Sh. 100,000 kutokana na ukata unaowakabili kwa sasa.

Ombi hilo liliwasilishwa jana katika Wizara ya Madini wakati wa kikao cha pamoja cha wanunuzi hao kilichofanyika kwa lengo la kujadili matatizo mbalimbali yanayowakabili, ikiwamo tozo kubwa.

Akiwasilisha ombi hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi wa Madini Taifa, Jeremiah Kituyo, alisema wazo la kutaka kushushwa kwa viwango hivyo, linalenga kumwezesha kila mfanyabiashara kumudu gharama hizo, hasa kutokana na biashara hiyo hivi sasa kutokuwa nzuri.

“Gharama za kulipia leseni ni kubwa, jambo ambalo linachangia wengi wetu kushindwa kumudu gharama za kulipia leseni. Wengi wetu tunapitia hali ngumu na mzunguko wa pesa kwa sasa ni mdogo kwenye soko la madini.

“Pamoja na tatizo hilo, tuna matatizo mengine ya leseni tunayopewa inatumika katika mkoa mmoja tu, hivyo ukienda kufanya biashara mkoa mwingine, inakulazimu kukata leseni nyingine.

"Jambo hilo linatupa shida kubwa sana, tunaomba serikali kupitia Wizara ya Madini kuhakikisha leseni moja inayotolewa itumike kwa mikoa yote," aliwasilisha.

Akizungumzia kilio hicho, mfanyabiashara mdogo wa madini, Abasi Mtunguja, alisema gharama ya leseni ni kubwa kulinganishwa na biashara wanayofanya kwa sasa.

"Tunatakiwa tuwe tumelipa ada hiyo ya leseni hadi kufikia Julai Mosi mwaka huu. Tunaomba muda uongezwe maana tumeambiwa ambaye hana leseni, hatakiwi kufanya biashara ya madini kabisa, jambo ambalo tunaomba serikali yetu itusikilize na kutuongezea muda wa kulipia huku ikipunguza kiwango hicho pia.

Habari Kubwa