Waomba kuboreshewa skimu ya umwagiliaji

25Oct 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Waomba kuboreshewa skimu ya umwagiliaji

WAKULIMA wa Bonde la Utengule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wameiomba serikali kuwaboreshea Skimu ya Umwagiliaji ya bonde hilo kwa kusakafia mfereji ili kuepusha upotevu wa maji unaosababisha migogoro baina yao.

Wakizungumza na Nipashe juzi, wakulima hao walisema chanzo cha skimu hiyo ambacho ni Mto Nzovwe kina maji mengi, lakini kutokana na mfereji huo kutosakafiwa mengi yanapotea njiani na kusababisha upungufu kwenye mashamba.

Mmoja wa wakulima hao, Yohana Mwazyunga, alisema wakulima wamekuwa wakigombania maji mara kwa mara kutokana na kiasi kinachofika mashambani kutokidhi mahitaji na njia pekee ya kuondoa migogoro hiyo ni kuiboresha skimu.

Alisema wakati mwingine huwa wanalazimika kuweka mgawo wa maji ili wakulima wamwagilie kwa awamu, lakini bado hayatoshelezi huku mwamko wa wakulima kulima kilimo cha umwagiliaji ukiongezeka.

“Huu mfereji una urefu wa zaidi ya kilomita 10, lakini ukisakafiwa angalau kilomita tano tatizo litakuwa limepungua kwa kiasi kikubwa, ukienda kwenye chanzo unakuta maji tuliyochukua ni mengi, lakini yanayofika huku mashambani ni kidogo sana,” alisema Mwazyunga.

Naye Godlove Huruma, Mwenyekiti wa kikundi cha vijana wanaolima vitunguu katika bonde hilo, alisema wakati mwingine wanalazimika kulala mashambani ili wamwagilie usiku kwa kuwa watumiaji wa maji wanakuwa wachache.

Hata hivyo, alisema kwa sasa watu wengi wamegundua mbinu hiyo hali ambayo bado inasababisha migogoro ya kugombea maji huku akidai kuwa muda wa usiku hata usalama huwa ni mdogo.

“Humu mashambani ni hatari sana nyakati za usiku maana kama unavyojua huo ni muda ambao unaweza ukang’atwa na nyoka au hata kama una adu yako anaweza akautumia muda huo kukuvizia na kukudhuru,” alisema Godlove.

Alisema baadhi ya wakulima wenye mitaji mikubwa wamekuwa wakitumia mashine kuvuta maji kutoka Mto Nzovwe, lakini kwa vikundi vya vijana kama cha kwao ambavyo havina mitaji inakuwa vigumu.

Habari Kubwa