Waomba maofisa kilimo kukabili wadudu

10Jan 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Waomba maofisa kilimo kukabili wadudu

BAADHI ya wakulima wa mahindi, wamewaomba maofisa kilimo kuwasaidia kukabiliana na wadudu walioanza kushambulia mahindi yakiwa shambani na kusababisha yasikue hali ambayo inaweza ikawaingiza hasara.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wakulima hao walisema wadudu hao aina ya Kanitangaze, wanakula mahindi kuanzia yakiwa madogo mpaka yatakapokuwa yamezaa na hawasikii dawa ya aina yoyote.

Mmoja wa wakulima hao, Joseph Mwashitete, mkazi wa Utengule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, alisema ili kuwadhibiti wadudu hao inatakiwa kupulizia dawa kila wiki na kwamba ukichelewa wanakula kiini cha mhindi na kuufanya udumae.

Alisema hakuna dawa ambayo imethibitishwa na wataalamu kuwa inawaua wadudu hao na hivyo wakulima wanalazimika kwenda kununua sumu za aina yoyote kwenye maduka na kupulizia hali ambayo wakati mwingine hazileti matokeo.

“Hawa wadudu mwanzoni walikuwa wanakula zaidi nyanya na wakulima tumeingia hasara sana na baadhi waliacha kabisa kulima nyanya, sasa hivi wamevamia mahindi, kila ukipiga dawa ni lazima ufanye kazi ya kwenda kuchunguza kama wamekufa,” alisema Mwashitete.

Alisema wadudu hao wanashambulia zaidi mazao wakati huu ambao mvua inanyesha kwa kufululiza kwa madai kuwa mvua inapunguza nguvu ya dawa wanazotumia.

Naye Jerome Mbozyo, kutoka Ilota katika Kata ya Mshewe Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, alisema wataalamu wa kilimo hawawatembelei katika maeneo yao kwa ajili ya kuangalia changamoto wanazokabiliana nazo kwenye kilimo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanaamua kuanza kubuni wao wenyewe namna ya kukabiliana nazo hali ambayo wakati mwingine wanashindwa kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya njia za kupambana na visumbufu vya mimea.

“Kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza mapinduzi ya viwanda ndicho kilifaa tuwe na maofisa kilimo katika kila kijiji, lakini sasa bado hawapo na sisi tunalima kwa kutumia uzoefu wetu hali ambayo inatufanya tusipate tija,” alisema Mbozyo.

Hata hivyo alisema wadudu aina ya Kanitangaze walianza miaka ya hivi karibuni, na kwamba kabla ya hapo walikuwa wanakabiliana na changamoto za kawaida.

Mmoja wa maofisa kilimo wastaafu anayeishi katika Kata ya Nsalala kwenye Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kwa sasa maofisa kilimo wana utaalamu wa nadharia badala ya vitendo na hivyo hawawezi kuwasaidia wananchi.

Alisema baadhi ya maofisa hao wanashindwa hata kulima mashamba yao na kwamba ikitokea akalima hatumii utaalamu unaotakiwa na hivyo kuwafanya wakulima kushindwa kujifunza kwao.

Alisema kwa sasa wakulima wanaona ni vema wakajifunze kwenye mashamba darasa ya kampuni za kuzalisha na kusambaza pembejeo za kilimo kuliko kwa hao maofisa kilimo.

Habari Kubwa