Waomba ruzuku ya kunusuru kaya maskini iongozwe

22Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nachingwea
Nipashe
Waomba ruzuku ya kunusuru kaya maskini iongozwe

WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, wamekiri kuwa mpango huo umekuwa mkombozi mkubwa kwao kutokana na kuwabadilisha kimaisha.

waziri wa kilimo, mwigulu nchemba.

Hata hivyo, wameiomba serikali kuongeza kiwango cha ruzuku ili kilingane na thamani halisi ya fedha kwa sasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na timu ya waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya wanufaika hao jana, walisema kiwango kinachotolewa ni kidogo mno ambacho pia hutolewa kila baada ya miezi mitatu.

"Hivyo serikali ione uwezekano wa kuongeza kiwango hicho na kutolewa kila mwezi," alisema Samson Nachuruchonga, ambaye ni mlemavu wa viungo mkazi wa kijiji cha Ntila.

Nachuruchonga alisema hata hivyo licha ya kwamba kiwango wanachopata kuwa ni kidogo, kimewasaidia kugharimia mahitaji muhimu ikiwamo chakula, kusomesha watoto wake kwa kuwanunulia sare na vifaa vya shuleni.

Alisema pia anazitumia fedha hizo kwa kilimo kwani kwa sasa anaweka watu shambani na kuwalipa, hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kutumia fedha zinazopatikana kupitia kilimo kujijengea nyumba ya bati.

Naye Zainabu Mpunga (73), mkazi wa kijiji cha Chiganga ambaye licha ya kuwa mjane pia anatunza wajukuu wake wawili ambao ni watoto wa marehemu binti yake, alisema kuwa ameanza ujenzi wa nyumba kwa kununua bati moja moja kila anapopata ruzuku hiyo na kuwa anatarajia mwaka huu ataanzisha ujenzi huo.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Tasaf wilayani Nachingwea, James Mbakile, alisema kutokana na mpango huo, baadhi ya wanufaika wamebadilisha maisha yao kwa kujianzishia miradi midogo midogo ikiwamo ufugaji wa kuku wa kienyeji, nguruwe na mbuzi na kujijengea nyumba za kisasa.

Alisema jumla ya Sh. bilioni 2.3 zimenufaisha kaya 5,850 katika vijiji 69 vya wilayani Nachingwea kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini tangu kuanza kwake.

Alifafanua kuwa wanufaika wake ni kaya za wazee wasiojiweza na wenye magonjwa sugu na wamekuwa wakishauriwa kutumia fedha hizo kidogo kwa kujitafutia chakula, kugharimia masomo na matibabu.

Aidha Ofisa Mshauri wa kitaalam wa Tasaf wa wilaya hiyo, Dorothy Shiyo, aliwaomba viongozi wa serikali za vijiji wawe wasimamizi wa karibu kwa kuwasimamia wananchi kutumia fedha wanazozipata kwa manufaa ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba.

Habari Kubwa