Waomba serikali kusikiliza ushauri wa wataalamu

23Mar 2019
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Waomba serikali kusikiliza ushauri wa wataalamu

WAFANYABIASHARA wa mazao na baadhi ya wadau wa mazingira katika Mkoa wa Kilimanjaro wameiomba serikali kusikiliza ushauri wa wataalamu wa viumbe kuhusu taarifa ya kuwepo kwa hatari ya kutoweka nyuki wanaochavusha mimea ya mazao ya chakula na biashara.

Mfanyabiashara wa mazao ya chakula, William Majaliwa, alisema utabiri wa wataalamu hao ni muhimu kuzingatiwa kwa sasa ili kulinda afya za walaji na mustakabali wa kizazi kijacho.

Mwingine aliyeomba kutazamwa upya tahadhari hiyo ni Witness Zablon ambaye ni mdau wa mazingira katika mji wa Moshi aliyedai kama hakuna nyuki, kunaweza kuwapo kwa matishio ya baa la njaa miaka ijayo.

Wiki iliyopita, mtaalamu wa nyuki nchini, Dk. Henry Njovu, alinukuliwa na gazeti hili alisema kuwa nyuki wanaosaidia uchavushaji katika mimea inayozalisha chakula na mazao ya biashara hapa nchini wako katika hatari ya kutoweka kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kemikali za viwandani wakati wa msimu wa kilimo.

Akizungumza hayo katika kongamano la watafiti na wataalamu wa mazingira lililofanyika katika Chuo cha Kimataifa cha Usimamizi na Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania maarufu kama Mweka.

Kwa mujibu wa Dk. Njovu, matumizi ya dawa za kemikali katika mashamba ya kilimo husababisha nyuki kufa na kuweka viumbe hivyo katika hatari ya kutoweka.

“Tatizo la uharibifu wa mazingira limeathiri kwa kiasi kikubwa nyuki hawa kwa asilimia 90 ambao kimsingi ndio wanaotegemewa kwa ajili ya uchavushaji wa mazao ya chakula na biashara.

“Hivi sasa wako katika hatari ya kutoweka kwa sababu ya kuwapo kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi na wakulima kutumia kemikali za viwandani msimu wa kilimo.”

Kutokana na hatari hiyo, Dk. Njovu ameeleza kuwa nyuki hao kwa sasa wameanza kupotea duniani na kwamba nchi ya China kwa sasa wanategemea binadamu kufanya shughuli za uchavushaji, jambo ambalo kwa nchi zinazoendelea litakuwa gumu kutokana na kutumia gharama kubwa.

Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Japhary Kidegesho, alieleza kuwa kama hatua za haraka za kuhifadhi nyuki hazitachukuliwa kuna hatari ya nchi kukumbwa na baa la njaa kutokana na wadudu hao wanaotegemewa kwa ajili ya uchavushaji wa mimea na miti kutoweka.

Hata hivyo, Mkufunzi mmoja wa chuo hicho, Dk. Oliver Nyakuga, amesisitiza kuwa kutokana na hali hiyo, bado elimu inahitaji kwa wananchi kuhusu umuhimu wa nyuki na kwamba mbali na upatikanaji wa chakula, wadudu hao ambao ni muhimu kwa maisha ya kibinadamu.

Andiko la Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) kuhusu umuhimu wa nyuki pia linasema, ‘uhai wa nyuki ni ustawi wa binadamu.’

FAO inaeleza wazi kuwa zaidi ya asilimia 75 ya chakula kinachozalishwa duniani kinategemea wadudu wachavushaji maua kama vile nyuki ambao hata hivyo uwepo wao duniani uko hatarini.

Habari Kubwa