Waonywa kuolea   fedha za korosho

05Dec 2017
Stephen Chidiye
Nipashe
Waonywa kuolea   fedha za korosho

MWENYEKITI wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma  (Tamcu), Hashim Mbarabara, amewataka wakulima wa korosho  kuondokana na tabia ya kuoa na kuacha wanawake pindi wanapouza mazao. 

Mbarabara alitoa elimu hiyo ya matumizi mazuri ya fedha wakati akizungumza na wakulima wakati wa mnada wa tatu wa mauzo ya korosho katika kijiji cha Amani kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani  msimu wa 2017/2018.   Mbarabara alisema badala ya fedha watakazozipata kuzitumia kuoa wanawake wapya na kuwaacha waliolima nao korosho hizo, badala yake wazitumie kujengea nyumba za kisasa na kuboresha makazi yao.  Alisena  matumizi mengine yanayoweza kuwaletea tija katika familia zao ni kusomesha watoto na kulipia bima za afya  ili kutibiwa kwa uhakika mwaka mzima pamoja na kununua pembejeo ambazo zitawasaidia kuhudumia mashamba yao msimu ujao. Takwimu za mauzo ya korosho katika minada iliyofanyika wilayani humo, zilizotolewa na Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Tawi la Tunduru, Japhary Matata, zinaonyesha  tani 13,743,683  zenye dhamani ya Sh.  49,968,087,547.00 zimeshauzwa kupitia minada mitano iliyofanyika tangu kufunguliwa kwa msimu wa 2017/2018.

 Matata alifafanua kuwa baadhi ya fedha zitakwenda kwa wakulima na kiasi kidogo zitainufaisha halmashauri ya wilaya hiyo kupitia ushuru wa Sh. 43.50 kwa kila kilo moja atakayouza mkulima,  vyama vya ushirika vitapata Sh. 90, Mfuko wa kuendeleza Zao la Korosho Tanzania (CIDTF) Sh.10 na  gharama za usafiri wa korosho hizo  kulingana na umbali wa eneo ambalo chama kipo pamoja na mchango wa elimu Sh. 30 kwa kila kilo moja aliyouza mkulima.