Wasambaza magogo walilia malipo Sao Hill

10Dec 2016
George Tarimo
MAFINGA
Nipashe
Wasambaza magogo walilia malipo Sao Hill

BAADHI ya wasambazaji wa magogo Sao Hill, Mufindi mkoani Iringa, wameilalamikia kampuni hiyo kwa kutowalipa fedha zao kwa wakati kama walivyokubaliana, hali ambayo imewafanya kuingiwa na hofu ya kuuziwa mali zao na taasisi za fedha kutokana na mikopo waliyochukua.

Wakizungumza na Nipashe juzi kwa nyakati tofauti, wasambazaji hao walisema awali walikuwa wakiingiza nguzo kwenye kampuni hiyo na walikuwa wakilipwa kwa wakati, lakini baadaye hali ilibadilika malipo yakawa yanasuasua.

Fitina William alisema kutokana na hali hiyo, ameathirika kwa kiasi kikubwa kwa sababu fedha za mtaji amechukua benki na hadi sasa hajarejesha kwa wakati husika.

“Awali walinitumia ujumbe mfupi wa simu kuniarifu kwamba nikiingiza mzigo kabla ya saa sita mchana nitalipwa siku hiyo hiyo.

Nilifanya hivyo na kulipwa, lakini mara nyingine niliingiza wakasema nitalipwa baada ya wiki na baadaye wakasema nitalipwa Desemba 6, mwaka huu na hawajanilipa tena hadi leo (juzi).

Wale watu niliokopa fedha wamenifuata hadi nyumbani,” alisema.

Naye Obed Dandi alisema amepata usumbufu mkubwa wa ahadi ambazo hazitekelezeki kutokana na kuzungushwa malipo yake wakati ameshapeleka mzigo kama walivyokubaliana.

“Tumepewa ahadi kila siku kuhusu malipo na tarehe ya mwisho kulipwa ni Desemba 8 (juzi) na leo (juzi) asubuhi tumefika hapa na tukapewa notisi ya tarehe ya kila mmoja anayostahili kulipwa.

Wengine wamevushwa hadi mwakani sasa tunashindwa kuelewa kama ndiyo hivyo, sisi ambao tulitakiwa kurejesha wiki iliyopita itakuwaje na ndiyo maana tunakosa imani na kampuni hii pamoja na tarehe waliyotuambia. Tunachokitaka ni fedha zetu,” alisema Obed.

Pamoja na kupangiwa tarehe, alisema kinachowasumbua zaidi ni mikopo waliyochukua benki na kutokana na ucheleweshaji huo wanapoteza imani katika taasisi walizokopa.

“Huenda tusipewe mikopo kwa kipindi kingine. Kwa msingi huo tumejenga migogoro na watu wengine kwa sababu wengine wamechukua kwenye vikundi na kuvunja uhusiano na majirani,” alisema.

Luta Maginga alisema kwa sasa amefikisha miezi miwili bila kulipwa huku akishutumu uongozi wa kampuni hiyo kwamba wanapofika kwa ajili ya kudai malipo yao wanazuiwa na walinzi huku uongozi ukijificha.

“Mimi kwangu ni Dar es Salaam, nadaiwa na taasisi za fedha, nimeshindwa kuendesha familia yangu kwa sababu kampuni hii haijanilipa fedha zangu na si mimi tu hata wengine ndoa zao zimevunjika,” alidai Maginga.

Nipashe ilimtafuta Meneja Mkuu wa Sao Hill, Vitus Bahati, ambaye alisema tatizo si kubwa kama wanavyodai wasambazaji hao.

“Sisi ndio kampuni peke inayonunua nguzo kwa kipindi hiki katika eneo hili na pia tunahudumia kampuni nyingine zinazozalisha nguzo kwa hiyo wao walileta mizigo mikubwa wakazidi uwezo wa kuwalipa,” alisema.

“Tunawaamini ni wadau wetu, tulikuwa tukiwasiliana nao kwa sms na kuwapigia simu za kiganjani kwa lengo la kuwaeleza hali halisi, lakini pia kwa sasa mauzo kwenye soko yamepungua.

Hata kwenye yadi zetu bidhaa zimejaa, hazitoki kwa sasa na wanaamini ni kwa sababu ya kipindi cha sherehe za sikukuu na mwezi Januari wanafunzi wanaenda shuleni kwa hiyo watu wanaofanya mambo ya ujenzi hawafanyi kama inavyotakiwa,” alisema Bahati.

Alisema wana changamoto kubwa kwa sababu mteja wao mkubwa ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambaye naye ana majukumu makubwa kutokana na hali ya kifedha, hivyo mara nyingi kutolipwa kama wanavyotarajia.

Habari Kubwa