Washauri wakulima kupunguziwa gharama

24Jul 2021
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Washauri wakulima kupunguziwa gharama

WANAFUNZI wa Kitanzania wanaosoma Chuo Kikuu cha Kilimo cha China (CAU), wameiomba serikali kuangalia namna ya kuwapunguzia gharama ya uzalishaji wakulima ili kuendana na kipato chao.

Chuo hicho kinatekeleza mradi wa pamoja wa kupunguza umaskini kwa wakulima wadogo mkoani morogoro.

Wanafunzi hao wanaosoma kwa njia ya mtandao kutokana na changamoto ya usafiri iliyosabishwa na ugonjwa wa corona, walitoa rai hiyo juzi baada ya kufanya ziara ya mafunzo kwa vitendo katika vijiji mbalimbali vinavyotekeleza mradi huo mkoani hapa.

Ziara hiyo ililenga kuangalia namna chuo hicho kinavyotekeleza miradi mbalimbali hasa ya kilimo cha mahindi katika kusaidi kuwapunguzia wakulima umaskini kwa utoaji mafunzo ya uzalishaji wa mazao kwa tija.

Mmoja wa wanafunzi hao, Juliet Frank, alisema licha ya mradi huo kuwanufaisha wakulima wengi baada ya kupata elimu ya kilimo cha kisasa, kuna haja ya wataalam kuangalia namna bora ya kuwapunguzia gharama za uzalishaji.

Mwanafunzi huyo aliomba serikali ya mkoa kwa kushirikiana na chuo hicho kinachotekeleza mradi wa pamoja endapo gharama zitapungua zaidi katika uzalishaji zitasaidia kupunguza umaskini kwa wakulima wadogo hasa kupitia kilimo cha mahindi.

“Licha ya mradi huu kuwasaidia wakulima wadogo, kuna kila sababu ya kutafuta njia mbadala ya kuwasaidia wakulima kupunguza mzigo wa kazi, kuwapo na vitendea kazi kama mashine za kupandia na kupalilia mahindi kama ilivyo katika mazao mengine. Hii itasaidia kuokoa muda,” alisema.

Naye Mwanafunzi Salma Shehe, alisema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa wakiwaathiri wakulima wadogo pale mvua zinapokosekana au kuzidi kiwango na kusababisha mazao kuharibika yakiwa shambani, hivyo kuwasabishia hasara.

Awali, Mratibu wa mradi huo, Ernest Mkongo, alisema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka 2011 kwa kuanza na kijiji cha Peapea wilayani Kilosa na baadaye kuhamishiwa katika kijiji cha Mtego wa Simba wilayani  Morogoro mwaka 2014.

Mkongo alisema kupitia mradi huo, wakulima walijifunza njia za kisasa na kuwawezesha kuvuna magunia 18 ya mahindi kwa ekari moja kulinganisha na awali wakivuna magunia manne hadi matano kwa ekari moja.

“Teknolojia walizofundishwa zimesaidia kuongeza tija kwa kiasi kikubwa mara tatu zaidi ya awali. Mkulima alikuwa anaambulia magunia matano pekee kwa ekari moja na kubwa zaidi elimu ile haikuishia kwa wanufaika wachache bali hadi wanakijiji wengine ambao walijifunza kupitia kwa wenzao,” alisema Mkongo.

Alisema baada ya mafanikio katika majaribio hayo, mradi ulipanuka na kuvifikia vijiji nane kutoka katika wilaya zote za Mkoa wa Morogoro katika kipindi cha mwaka 2018 hadi mwaka 2021.

Mkongo alivitaja vijiji vingine na wilaya zake kwenye mabano ni Letugunya na Ngayaki (Gairo), Kitete (Kilosa) , Kisegese (Kilombero) , Kiswago (Malinyi), Kikundi (Morogoro), Makuyu (Mvomero) na Mwaya, Wilaya ya Ulanga.