Washindi droo Exim wajizolea fedha, gari

26Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Washindi droo Exim wajizolea fedha, gari

BENKI ya Exim imetangaza washindi wa droo ya kwanza ya kampeni  ya ‘Weka Mkwanja Tukutoe!’inayoendeshwa na benki hiyo, ikilenga kuhamasisha Watanzania kujiwekea amana, huku wakinyakua zawadi mbalimbali ikiwamo fedha taslimu na gari aina Toyota Vanguard.

Meneja Masoko na Mawasiliano Msaidizi wa Benki ya Exim, Mariamu Mwapinga (kushoto), akiwaonyesha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, zawadi kubwa ya gari aina ya Toyota Vanguard, itakayotolewa kwa mshindi wa kampeni  ya ‘Weka Mkwanja Tukutoe!’ inayolenga kuhamasisha Watanzania kujiwekea amana kupitia benki hiyo. Wengine ni ofisa kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Neema Tatock (wapili kushoto) na maofisa  wa benki hiyo. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Akitangaza washindi wa droo ya kwanza ya kampeni hiyo iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko na Mawasiliano Msaidizi wa Benki hiyo, Mariam Mwapinga, alisema jumla ya washindi sita walipatikana kupitia droo hiyo na kujishindia zawadi ya shilingi milioni sita fedha taslimu.

“Katika droo ya leo jumla ya washindi sita wamepatikana na wameweza kujishindia zawadi za fedha taslimu shilingi milioni sita. Washindi hawa sita watakabidhiwa zawadi zao katika maeneo yao waliopo na tutaendelea na droo kama hizi kila mwezi na washindi wataendelea kuingia kwenye droo itakayowawezesha kushinda zawadi kubwa ya gari aina ya Toyota Vanguard.’’

“Wateja wetu wa sasa na wale wapya watakuwa kwenye nafasi ya kujishindia zawadi hizi kila wakapojiwekea akiba ya kuanzi shilingi 500,000 na kuendelea. Kadili wanavyojiwekea amana kubwa zaidi ndivyo wanavyojiweka kwenye nafasi ya kushinda zawadi kubwa zaidi,’’ alisema Mariam wakati wa droo hiyo iliyohudhuriwa pia na mwakilishi kutoka  Bodi ya Michezo ya Kubahatisha nchini.

Akifafanua zaidi kuhusu kampeni hiyo, Mariam alisema inalenga kuleta mabadiliko kwenye mtazamo wa uhifadhi wa amana miongoni mwa Watanzania kutoka kuhifadhi pesa majumbani na badala yake wazihifadhi kupitia benki hiyo kwa usalama wa fedha zao sambamba na faida nyingine nyingi ikiwamo riba.

“Lengo si tu kuhamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kujiwekea amana, tunachohitaji ni kuona kwamba Watanzania wengi wanajiwekea amana zao sehemu salama ili kujiendeleza kukua kiuchumi ndio maana tumejipanga kuwahamasisha watumie akaunti zetu mbalimbali ikiwamo akaunti ya mshahara inayotumika kwa matumizi mbalimbali ya kila siku,” alisema.

Habari Kubwa