Wasikitika mradi wa umwagiliaji

05Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe
Wasikitika mradi wa umwagiliaji

WADAU wa uzalishaji wa mazao ya chakula katika skimu ya umwagiliaji ya soko Wilaya ya Moshi, wameeleza masikitiko yao kuhusu mradi wa uimarishaji wa skimu hiyo kutengewa Sh. milioni 150 ambazo hauwezi kukidhi mahitaji ya kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda.

Skimu hiyo yenye wakulima zaidi ya 270, inahudumiwa na wananchi wa vijiji vitatu vya Kiterini, Soko na Kyomu.

Baadhi ya wakulima walitoa dukuduku lao juzi, ikiwa ni siku chache baada ya kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kupita eneo hilo la Kata ya Kahe Mashariki na kutoa maelekezo kwa serikali kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya kuboresha skimu hiyo ili kuondoa malalamiko ya wakulima.

Mmoja wa wakulima hao, Kabanga Alli, alisema kilimo cha umwagiliaji ili kiwe endelevu na chenye tija kuweza kufikia Tanzania ya viwanda, uwekezaji wa miundo mbinu ya kisasa, mitaji, maofisa ughani na uwezeshwaji kiuchumi wa wakulima wenye mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa.

Rehema Mgonja alisema: “Ukitazama kiasi cha fedha ambacho serikali imewekeza nadhani bado ni kidogo, ikilinganishwa na mahitaji ya viwanda vyetu hasa vya kuongeza mnyororo wa thamani mazao ya mpunga, mbogamboga na mahindi. Tunashauri serikali kwa maana ya halmashauri yetu kuongeza fungu la kuimarisha miundombinu ya skimu ya soko.”

Greyson Badueli alisema pamoja na uwekezaji huo, wakulima wanaomiliki vitalu katika skimu ya soko, hawajapewa elimu ya kutosha ya kujiunga katika vyama vya umwagiliaji.

Alisema jambo hilo kama litafanywa na watendaji wa serikali, litasaidia wakulima kusimamia na kuihudumia vyema miundo mbinu ya umwagiliaji ili iwe endelevu kwa kulipia ada za uendeshaji, matunzo na matumizi ya maji.

Juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Kastori Msigala, akizungumza na wakulima hao, alisema mradi huo unaendeshwa na umoja wa wakulima wa umwagiliaji soko (Uwaso) na una jumla ya wakulima 270.

Sheria ya Umwagiliaji, Namba 5 ya Mwaka 2013, na Kanuni zake za Mwaka 2015, inahamasisha skimu za umwagiliaji kusimamiwa na kuendelezwa na vyama vya umwagiliaji ili ziweze kuwa na ufanisi zaidi.

Alisema chanzo cha maji ya skimu hiyo ni mto soko na kwamba zao kuu linalolimwa katika skimu hiyo ni zao la mpunga na mazao mengine ni mboga mboga, matunda na mahindi.

Alisema eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni hekta 400 na kwamba hadi sasa, eneo lililoendelezwa ni hekta 270 sawa na asilimia 67.5.

Habari Kubwa