Wataka kampuni za madini kulipia kodi mkoani

17Jan 2017
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
Wataka kampuni za madini kulipia kodi mkoani

WAFANYABIASHARA katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kuzishinikiza kampuni mbili za uchimbaji madini kulipia kodi mkoani humu badala ya Dar es Salaam.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza makali ya Sh. bilioni 12 ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Ruvuma imepangiwa kukusanya mwaka huu kutoka kwa wafanyabiashara.

Ombi hilo lilitolewa na wafanyabiashara hao kwenye mkutano uliofanyika baina yao na uongozi wa TRA Makao Makuu uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Songea Club mjini hapa jana.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Jaribuni Mangoma, alisema kuwa kutokana na kitendo cha serikali kuziachia kampuni hizo mbili (majina yamehifadhiwa), ndiko kunakowafanya wafanyabiashara kukadiriwa kodi kubwa inayowafanya baadhi yao wafilisike.

Mangoma alisema kuwa ifahamike kuwa Mkoa wa Ruvuma hauna hata kiwanda kimoja, lakini TRA wameweka makadirio makubwa yanayosababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao kutokana na kushindwa kumudu kodi waliyokadiriwa.

Mfanyabiashara mwingine, Omary Chika, alilalamikia kuwapo kwa mrundikano wa kodi unaonekana kuwa kero.

Chika aimeshauri TRA kuona umuhimu wa kuwa na tozo moja kwa kila mfanyabiashara ambalo litaunganiisha kodi zote zinazotolewa hivi sasa kwa lengo la kupunguza kero wanayoipata wafanyabiashara hao.

Naye mfanyabiashara Emmanuel Kondowe, ameishauri serikali kufanyia marekebisho sheria ya kuwatoza wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni na hoteli kwa kulipa kodi kwa vigezo vya dola badala ya fedha ya Kitanzania, jambo alilosema huleta mgogoro baina ya wafanyabiashara na TRA ambayo huwalazimisha walipe kwa dola wakati baadhi ya wateja wao hawana uelewa wa matumizi ya dola.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Ruvuma, Wilson Nziku, alisema kuwa jamii ya wafanyabiashara hapa nchini bado haina uelewa wa kutumia mashine za kielektroniki (EFD).

Kwa msingi huo, Nziku ameiomba serikali kutoa muda maalum kwa TRA kutoa elimu ya kutosha.

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichele, aliwataka wafanyabiashara hapa nchini kuona umuhimu wa kulipa kodi.

Habari Kubwa