Wataka maeneo kupisha ujenzi reli 

03Dec 2017
Peter Mkwavila
Nipashe Jumapili
Wataka maeneo kupisha ujenzi reli 

WAFANYABIASHARA wanaofanya shughuli zao kwenye hifadhi ya reli Manispaa ya Dodoma,  ambao vibanda vyao vitabomolewa wameiomba  serikali kuwaongezea muda wa kuhamisha mali zao na kuwatafutia eneo la kudumu kwa ajili ya biashara zao.

 Wafanyabiashara hao wanatakiwa kupisha eneo hilo linalotarajiwa kujengwa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa.

Katika ubomoaji huo,  wafanyabiashara wa stendi ya Jamatini, soko la Sarafina, vituo vya mafuta, mama lishe na mabanda ya kukatia tiketi za mabasi yaendayo mikoani,  watakumbwa na adha hiyo.

Ombi hilo walilitoa wafanyabiashara hao mbele ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alipokuwa akisikiliza kilio chao kutokana na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) kutaka kuyavunja mabanda yaliyoko kwenye eneo la hifadhi ya reli inayotakiwa kujengwa hivi karibuni.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Sakina Saidi, alisema hawapingani na serikali juu ya kupisha maeneo hayo kwa ajili ya maendeleo ya taifa, bali wanachohitaji ni kuonyeshwa sehemu watakayofanyia biashara zao wakati kampuni hiyo ikijiandaa kuanza kujenga reli hiyo.

“Mkuu wa Mkoa tunaiheshimu na kuitii serikali yetu tukufu chini ya uongozi wa Rais  John Magufuli.

Tunachokuomba tupatiwe muda na tuonyeshewe maeneo  tutakayofanyia biashara zetu, ukizingatia kuwa wengi tumechukua mikopo inayotuwezesha kufanya shughuli hizi za biashara na hata kulipia ada watoto wetu” alisema.

Jonath Jonathani  ambaye ni mjasiriamali wa stendi ya Jamatini, alisema hawana sababu ya kubishana na serikali inapoamua kufanya mabadiliko ya kimaendeleo bali kinachotakiwa kwa mamlaka husika ya manispaa ni kuwaonyesha eneo husika ili wafanye kazi zao.

Baada ya kusikiliza kilio chao, Dk. Mahenge aliwataka wafanyabiashra hao kutii amri ya kuondoka kwenye maeneo hayo ambayo kwa sasa tayari mkandarasi ameshaingia  mkataba wa kutaka kuanza kazi wakati wowote.

Dk.Mahenge alisema pamoja na kuwa wamewekeza mali zao  na wana mikopo, wajiandae  kuondoka kwenye eneo hilo ili kupisha kazi hiyo.

“Wakati serikali ikitafakari kuhusiana na suala hilo la sehemu ya kuwapangia eneo la kufanya shughuli zenu,hivi sasa zoezi la ubomoaji litabidi lisimame kwa muda ili na nyie mjiandae kuondoa mali zenu kwa usalama zaidi bila bughudha yoyote,” alisema.

"Kuanzia Jumatatu nitaomba kukutana na viongozi wenu ili tuwasiliane kwa ajili ya kuwapatia majibu yatakayokuwa sahihi yatakayowawezesha kujua hatima yenu juu ya kuondoka kwenu na mahali ambapo mtakapangiwa.” 

Habari Kubwa