Wataka w’biashara Kiwira kuondolewa maeneo ya hifadhi

07Jul 2020
Nebart Msokwa
Rungwe
Nipashe
Wataka w’biashara Kiwira kuondolewa maeneo ya hifadhi

WAFANYABIASHARA wa ndizi katika soko la Kiwira lililopo Tandale katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, wameiomba serikali kuwaondoa wafanyabiashara wenzao wanaouza kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara wakidai kuwa wanawazibia wateja.

Wanadai kuwa baada ya soko hilo kuanzishwa, serikali iliwaondoa kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara walimokuwa wanafanyia biashara na kuwapeleka katika eneo hilo, lakini baadhi wameendelea kubaki katika maeneo hayo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, James Mwakanyamale, alisema wao waliondolewa na serikali na wakala wa barabara nchini Tanroads wakaweka mabango ya kuwazuia kufanya shughuli zozote ndani ya hifadhi za barabara lakini wenzao bado wapo.

Alisema kitendo hicho kinawafanya wateja waishie barabarani badala ya kwenda kwenye soko ambako wao walihamishiwa na kuhakikishiwa kuwa wateja watakuwa wanaenda huko.

“Tuliambiwa tunahatarisha maisha yetu kwenye hifadhi ya barabara na ndio maana wakatuleta huku, sasa tunashangaa kwa nini wenzetu wanaendelea kuuzia hasa pale Kiwira,” alisema Mwakanyamale.

Naye Neema Mwaipopo, alisema kuna baadhi ya maofisa wa serikali wanaendelea kukusanya ushuru hata kwa wale wanaouzia kwenye hifadhi ya barabara badala ya kuwaondoa.

Alimwomba Mkuu wa Wilaya hiyo, Julius Chalya, kuingilia kati kwa maelezo kuwa biashara hiyo inasababisha migogoro baina yao na kwamba hata wao wanatamani kurudi kwenye maeneo yao ya awali ambayo waliondolewa.

“Hata sisi tunatamani kurudi na endapo serikali itaendelea kuwaacha walioko barabarani, hata sisi wenyewe tunaanza kurudi kidogo kidogo na hautakuwa utaratibu mzuri, tunamwomba Mkuu wa Wilaya atusaidie,” alisema Neema.

Katika maeneo yote ya barabara ambayo serikali iliwaondoa wafanyabiashara, Tanroads waliweka mabango ambayo yanawazuia wananchi kuendelea kufanya biashara kwenye maeneo hayo lakini kwenye baadhi ya maeneo bado wafanyabiashara wanaendelea kuuzia.

Habari Kubwa