Watakiwa kufuata mwongozo uhifadhi maeneo ya bahari

22Jun 2022
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Watakiwa kufuata mwongozo uhifadhi maeneo ya bahari

WANANCHI wametakiwa kufuata mwongozo uliotolewa na Idara ya Uhifadhi kwa taratibu za kisheria zilizowekwa na serikali ili kuepusha athari mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo ya hifadhi za bahari pamoja na upotevu wa vivutio vya utalii.

Hayo yalielezwa na Meneja wa Hifadhi ya Tumbatu (TUMCA), Said Shaib Said, kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi katika kikao na manahodha wa boti za kupeleka watalii katika maeneo ya hifadhi za bahari Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kutunza mazingira ya bahari ili kuufanya utalii kuwa endelevu.

Said alisema kuna baadhi ya wageni wana tabia ya kuwalisha vyakula holela viumbe vya baharini ikiwamo kasa na kuwabeba kwa ajili ya kupiga nao picha jambo ambalo ni kosa kisheria na kupelekea athari kubwa kuliko faida inayopatikana.

Alisema umefikia wakati kwa jamii kubadilika hususani wenye shughuli za kitalii kuacha tabia ya kutupa taka za plastiki katika hifadhi za bahari ili kukuza sekta ya uchumi wa buluu kuweka mazingira safi na salama kwa ajili ya afya ya baharini na ufukweni.

Naye Ofisa Mipango, Mchanga Said Khamis, kutoka Idara ya Uhifadhi wa maeneo ya bahari Zanzibar, alisema ushirikiano wa pamoja unahitajika kwa manahodha wa vyombo vya utalii kuepuka kutupa nanga katika matumbawe ili kuziacha rasilimali za bahari kuwa salama.

Mshauri wa uchumi wa buluu, Kris Horill, aliwataka manahodha wanaopeleka wageni katika maeneo ya hifadhi kuwa mstari wa mbele katika suala la ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari kutunza mazingira ya bahari ili kuleta mabadiliko katika sekta ya uchumi wa buluu kupitia utalii.

Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho wameziomba taasisi husika kuzidi kuwapatia elimu ya muongozo uliotolewa na idara ya uhifadhi kutokana na umuhimu wa kutunza viumbe wa baharini kwa ajili ya kutanua sekta ya utalii nchini na maendeleo kwa taifa.

Habari Kubwa