Watakiwa kutangaza fursa Bahari ya Hindi

17Sep 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Watakiwa kutangaza fursa Bahari ya Hindi

WADAU wa jumuiya ya nchi zilizoko kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi wametakiwa kuzitangaza fursa zilizoko nchini ili kuimarisha uwekezaji katika sekta ya uvuvi.

Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Mussa Haji Ali, wakati akifunga kikao cha siku tatu cha wadau wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi kilichofanyika Maisara Mjini Unguja.

Alisema fursa zilizopo katika Bahari ya Hindi ni nyingi ikiwamo uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ambao unaleta faida kubwa katika kukuza uchumi wa bluu nchini.

Alieleza kuwa, serikali inatambua umuhimu wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi hasa katika kuutangaza utalii ambao unasaidia katika kukuza uchumi wa taifa.

Alisema serikali zote mbili zinaendelea kufanya jitihada za kuimarisha matumizi bora ya bahari ikiwamo kupiga vita uvuvi haramu katika bahari ili kulinda uchumi wa bahari.

Aidha, katibu huyo alisema ziara zilizofanywa na wadau hao ya kutembelea kituo cha kutotolea vifaranga Kibweni na Mamlaka ya Bahari Kuu Fumba ziwe ni chachu ya kuibua mawazo mazuri yatakosaidia katika kufanikisha uchumi wa bluu nchini.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, Dk. Emmanuel Sweke, alisema ipo haja ya kuwahamasisha wazawa kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu ili rasilimali za taifa zitumike kuwanufaisha wananchi.

Alisema kuwa wawekezaji wengi wanaokuja kuwekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ni wageni, hivyo ipo haja ya kuwawezesha wazawa kimtaji ili kuwekeza.

Aidha, alipendekeza ujenzi wa bandari ya uvuvi nchini, ujenzi wa viwanda vya samaki, upatikanaji wa boti, na ufugaji wa samaki ufanyike nchini ili rasilimali ya bahari ilete manufaa makubwa zaidi kwa taifa na kuzalisha ajira kwa Watanzania.

Wadau wa jumuiya ya nchi zilizopo kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi walipata fursa ya kutembelea kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki Kibweni na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Fumba.