Watakiwa kutumia teknolojia ya kupukuchua mazao nafaka

24Nov 2020
Grace Mwakalinga
Njombe
Nipashe
Watakiwa kutumia teknolojia ya kupukuchua mazao nafaka

WAKULIMA wa mazao ya nafaka wanaotoka Mikoa ya Ruvuma, Iringa na Njombe, wametakiwa kutumia teknolojia ya kupukuchua mazao  kwa mashine ili kupunguza upotevu wa mazao na gharama ya kutumia idadi kubwa ya watu kupukuchua kiwango kidogo cha mazao. 

Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Njombe, Ayoub Mndeme,  aliyasema hayo wakati wa  uzinduzi wa teknolojia ya  upukuchuaji wa mazao ya nafaka kwa njia ya mashine ambayo ilifanyika mkoani humo.
 
Alisema licha ya  teknolojia hiyo kutumia watu  wachache  na kwa ufanisi,  ina uwezo wa kupukuchua kiasi kikubwa cha nafaka kwa muda mfupi hivyo kuwafanya wakulima wengi kuvutiwa kutumia mashine hizo.
 
Alisema mbali na teknolojia hiyo kurahisisha kazi, lakini inaweka usalama wa afya ya waendesha mitambo kutokana na miundombinu yake kutoruhusu vumbi kumfikia mtumiaji wakati wa zoezi la kupukua mahindi.
 
“Upatikanaji wa huduma hii ya kumrahisishia kazi mkulima anapovuna mazao yake  na miongoni mwa njia rahisi za kupata teknolojia hiyo ni kupitia mawasiliano ya simu ya mkononi ambapo muhitaji uzipata katika mfumo maalum,” alisema Mndeme.
 
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TAPBDS, Deodati Bernard, alisema waliamua kuleta mradi huo mkoani Njombe kwa sababu ni wadau wanaoshiriki kuendeleza wakulima katika kuhakikisha wanafanya kilimo biashara.
 
Alisema kupitia mradi wa kipato tija Tanzania ambao pia unasimamiwa na Agra umewakifika wakulima zaidi ya 30,000 tangu kuanzishwa kwake mwaka   2017.
 
“Zoezi la kupata wanufaika wa mashine hizo za mazao lilifanyika kwa kutoa tangazo na wakulima kuomba ruzuku ambapo idadi ya wakulima 57 walijitokeza na waliokidhi vigezo na kupatiwa mashine hizo ni 17 mashine ambazo zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 60,” alifafanua Benard.
 
Vilevile, wajasiriamali zaidi ya 250 wakiwamo vijana wanaofanya shughuli zao ndogo 30 waliwezeshwa zaidi ya milioni 60 katika mpango wa ruzuku na kuchangia  ongezeko la ajira zaidi ya vijana 350 katika mikoa hii mitatu ya Njombe, Iringa na Ruvuma.
 
Baadhi ya wanufaika hao wa mashine za kupukuchulia mazao ya nafaka akiwamo Lucy Kitavile na Ibrahim Mhesi walishukuru kupatiwa mashine hizo kwa ushirikiano wa AGRA na TAPBDS na kwamba  zitawawezesha kupukuchua kiwango kikubwa cha nafaka tofauti na awali ambapo ilikuwa inawalazimu kutumia nguvu kubwa kupukuchua kiasi kidogo cha nafaka.
 
“Nawashukuru AGRA na TPBDS kwa kuniwezesha kupata mashine za kupukuchua na guta la kubebea mazao kwani awali nilikuwa napiga mahindi kwa lutumia miti,” alisema Kitavile.
 
Mradi huo wa kupukuchua mazao kwa njia ya mashine ulianza Julai mwaka huu na unatarajiwa  kukamilika Desemba mwaka huu ambapo imeshirikisha mikoa ya Iringa, Njombe, Katavi, Ruvuma, Kagera na Mbeya.
 

Habari Kubwa