Watalii wafurahia wanyama Ngorongoro

15May 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Watalii wafurahia wanyama Ngorongoro

WATALII zaidi ya 200 kati ya 336 kutoka nchini China jana wametembelea Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na kufurahia wanyama mbalimbali waliowaona kwenye shimo kubwa lililopo hifadhi hiyo maarufu kwa jina la Kreta.

Baadhi ya kundi la watalii 336 kutoka nchini China wakiingia geti Kuu la Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro. Picha: Cynthia Mwilolezi, ARUSHA

Watalii hao waliwasili hifadhini hapo saa 5 :00 asubuhi wakitokea Arusha Mjini walikokuwa wamelala, kwa magari maalumu ya kitalii waliyoandaliwa nchini na kupokelewa kwa ngoma za asili za kabila la Kimasai na Watatoga.

Baada ya kuingia lango kuu la hifadhi walionekana wakiwa na furaha, huku baadhi yao wakionekana wakipiga picha msitu mnene waliouona na wanyama.

Aidha, walilazimika kushuka baadhi ya maeneo na kupiga picha kwenye miti mikubwa na magogo ya miti iliyolala.

Baadhi ya watalii hao walihudhuria kongamano la uwekezaji lililofanyika ukumbi wa kimataifa wa mikutano AICC uliopo Mjini Arusha, huku wenzao wakitangulia Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.

Awali Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroard International Holdings Groups ya China, He Lei Hiu, alisema wamefurahishwa na ukarimu wa Watanzania na mapokezi makubwa waliopatiwa.

Alisema katika ziara hiyo, jana wameanza kwa kutembelea vivutio vya utalii vya Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na kujionea wanyama wa kila aina waliowavutia.

Alisema leo watatembelea hifadhi ya Serengeti na baadaye wataenda Zanzibar kujionea vivutio vya asili vilivyopo Tanzania.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Hoteli ya Serena iliyopo Ngorongoro ambayo ilihudumia chakula cha mchana kwa wageni hao, Nickson Kanika, alipongeza serikali kufanilisha kuleta kundi kubwa la watalii toka China.

"Hatujawahi kupokea kundi kubwa la watalii toka China, lakini kwa jitihada za serikali kupitia wizara husika TANAPA na Bodi ya Utalii (TTB) wamefanikisha zoezi hili muhimu la kihistoria," alisema.

Alisema anaamini kwa ujio huo kila Mtanzania atanufaika kwa namna moja au nyingine kupitia fedha watakazoziacha kwa kununua vitu mbalimbali na kuangalia vivutio hivyo.