Watalii waongezeka licha tishio la corona

24Jul 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Watalii waongezeka licha tishio la corona

LICHA ya dunia kukabiliwa na janga la corona, idadi ya watalii walioingia Zanzibar kwa Juni, mwaka huu, imeongezeka na kufikia 20,416 ikilinganishwa na 9,280 walioingia Machi, mwaka huu.

Akitoa takwimu za uingiaji wa wageni kwa waandishi wa habari ofisini kwake Mzazini, Mkuu wa Takwimu za Kiuchumi kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Abdulrauf Ramadhani Abeid, alisema Ufaransa inaongoza kwa kuleta watalii wengi Zanzibar.

Alisema wageni 11,588 waliongia nchini ni kutoka Ulaya ambao ni sawa na asilimia 56.8.

Alisema kwa mwezi huo, Ufaransa iliongoza kwa kuleta wageni 2,232 sawa na asilimia 10.9 ya wageni wote ikifuatiwa na Poland 2,101 sawa na asilimia 10.3.

Wageni waliongia Zanzibar kwa kutumia usafiri wa boti kupitia Bandari ya Malindi, alisema walikuwa 5,152 sawa na asilimia 25.2 na waliongia kupitia viwanja vya ndege ni 15,264 sawa na asilimia 74.8.

“Asilimia 99.4 ya wageni walikuja kwa ajili ya mapumziko, asilimia 0.5 kwa ajili ya kuwatembelea ndugu na marafiki zao na asilimia 0.1 ya wageni walikuja kwa sababu zingine,” alisema Abeid.

Naye Dk. Estella Ngoma Hassan, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), alisema kuwako kwa idadi kubwa ya wageni kutoka Ufaransa kumetokana na nchi hiyo kuondoa vikwazo vya kusafiri katika nchi yao na kusababisha kuondoka nchini na kwenda nchi zingine. Alisema hali imesababisha Zanzibar kupata wageni wengi kutoka nchini humo.

Aidha, alisema sababu nyingine iliyofanya wageni kutoka Ufaransa kuwa wengi ni  pamoja na kuanza  chanjo ya corona nchini humo.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk. Abdulla Mohammed Juma, alisema kamisheni hiyo imebadilisha mikakati ya soko la utalii ambapo awali walikuwa wakitegemea watalii kutoka Ulaya.

Alisema mikakati hiyo imeanza kuzaa matunda na kwamba wageni mbalimbali wamekuwa wakiongezeka.

Pia alisema kuwa kwa miaka sita iliyopita nchi iliyokuwa ikiongoza kuingiza watalii kwa wingi Zanzibar ni Italia lakini kwa sasa idadi imepungua kutokana na corona.