Watanzania 4,000 kunufaika na ajira kiwanda cha nguo

20Dec 2016
Getrude Mbago
Nipashe
Watanzania 4,000 kunufaika na ajira kiwanda cha nguo

ZAIDI ya Watanzania 4,000 wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira kufuatia kiwanda kipya cha nguo kitakachojengwa mkoani Morogoro.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru.

Kiwanda hicho cha Mazava Fabric and Production kinachotarajia kuanza ujenzi wake mapema mwakani na kukamilika baada ya mwaka mmoja, kinatoa matumaini kwa vijana wengi wanaosota mitaani bila ajira.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka saba ya kiwanda hicho mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni matokeo ya juhudi za serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Dk. Meru alisema sasa vijana wengi wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa ajira kiasi cha kuwafanya waone maisha magumu, lakini uwapo wa kiwanda hicho utawakomboa wengi kuondokana na hali hiyo.

“Ninafurahi kuanzishwa kwa kiwanda hiki kitakachojengwa katika eneo la Uwekezaji la StarCity mjini Morogoro kwani kitasaidia kupatikana kwa ajira, vijana wengi hawana kazi, kwa hiyo baada ya kufunguliwa hapa, nafikiri ajira zitakuwa nyingi sana, " alisema Dk. Meru.

Kiwanda hicho cha Mazava Fabric & Production ni cha pili kujengwa na kampuni hiyo nchini.

Dk. Meru aliwahakikishia wawekezaji wote nchini kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kutatua vikwazo mbalimbali vya kiuwekezaji vikiwamo vya ushuru na kodi ili kuwavutia wawekezaji zaidi.

Aliwaasa wakulima wa pamba nchini kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwani vipo viwanda vingi vya nguo vitakavyojengwa na kutegemea rasirimali hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji na Mauzo ya Nje (EPZA) Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, alisema kazi kubwa ya mamlaka hiyo ni kuhamasisha uwekezaji katika kanda maalumu za kiuchumi, kuvutia na kuhamasisha uhuishaji wa teknolojia mpya, kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda usindikikaji wa malighafi zinazopatikana nchini, kutengeneza fursa za ajira na kuongeza pato la fedha za kigeni nchi.

Alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza na kuchangamkia fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini badala ya kuachia fursa hizo kwa wageni pekee.

Naye mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Winds Group Ltd wamiliki wa Mazava, Urban Geiwald alisema kuwa wataendelea kuongeza uwekezaji baada ya kuvutiwa na juhudi za serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za kiuwekezaji na hivyo kufanya mazingira ya uwekezezaji kuwa bora zaidi nchini.

Habari Kubwa