Watanzania kunufaika mafunzo gesi, mafuta

13May 2022
Getrude Mbago
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watanzania kunufaika mafunzo gesi, mafuta

WATANZANIA wanatarajiwa kunufaika na elimu kuhusu sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia itakayotolewa na wataalamu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwenye maonyesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi mkoani Morogoro.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella.

Wataalamu hao wamejipanga kukuza uelewa wa sekta hiyo ili kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye sekta husika.

Maonyesho hayo yalifunguliwa Mei 9 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella katika viwanja vya Jamhuri mkoani humo na yataendelea hadi Mei 14, mwaka huu, yakitarajiwa kuhitimishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Baadhi ya masuala yatakayozungumziwa kwenye banda la PURA ni pamoja na mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia, mnyororo wa thamani wa mradi wa kubadili gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zinazoendelea nchini.

Maeneo mengine ni ushiriki wa wazawa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli na fursa zinazopatikana kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Shigella alisema maonyesho hayo ni fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kazi na washiriki wengine kuhusu fursa mbalimbali na kero zinazowakabili na jinsi ya kukabiliana nazo.

"Maonyesho haya ni ya muhimu kwani yanatoa elimu kwa wananchi ambayo inawawezesha kushiriki kwa wingi na kwa ubora kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo,” alisema.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa, alisema maonyesho hayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu 'uchumi imara kwa maendeleo endelevu'.

Alisema lengo la maonyesho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu uwapo wa mifuko na programu za uwezeshaji, jinsi ya kujiwekea akiba na jinsi ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.

“Maonyesho haya pia yanalenga kutengeneza mtandao wa wafanyabiashara watakaoshiriki na kukuza masoko ya wajasiriamali ili kujiletea maendeleo," alibainisha.

Habari Kubwa