Wateja wa Tigo sasa kutoa fedha kwenye ATM za UmojaSwitch

22Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wateja wa Tigo sasa kutoa fedha kwenye ATM za UmojaSwitch

Kampuni ya simu ya Tigo kupitia kitengo cha Tigo Pesa imeingia ubia na taasisi ya UmojaSwitch (BCX) kwa kuzindua huduma ya kutoa fedha kwa njia ya ATM ambayo ni rahisi na ya uhakika kwa wateja wa Tigo.

Kaimu Mkuu wa kitengo cha huduma za Kifedha wa Tigo Pesa, Angelica Pesha akizindua huduma ya kutoa fedha kwa njia ya ATM, pembeni yake ni Afisa Mkuu Mtendaji wa UmojaSwitch,Company Ltd, Danford Mbilinyi, uzinduzi huu umefanyika leo Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika leo Oktoba 22,2019, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha huduma za Kifedha wa Tigo Pesa, Angelica Pesha amesema huduma hiyo mpya ni utekelezaji wa mkakati wa Tigo wa kutoa huduma za kidigitali zenye ubora ili kukidhi mahitaji ya wateja.

Amesema kuwa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili ni hatua muhimu katika kuchochea agenda ya ujumuishwaji wa watu kiuchumi kwani inaifanya huduma ya Tigo Pesa kuwa zaidi ya huduma ya kifedha kwa njia ya simu na kuwa huduma ya kibenki.

“Tuna furaha kuzindua huduma hii mpya ya kibenki ambayo itawapa wateja wetu uhuru wa kifedha kwakuwa ni njia rahisi na ya haraka ya kupata pesa mahali popote kupita ATM za UmojaSwitch zilizopo maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema Pesha.

Ameongeza kuwa huduma hiyo mpya itarahisisha utumaji na kupokeaji wa pesa kwa kutumia ATM za UmojaSwitch zaidi ya 350 zilizopo hapa nchini hivyo kuchochea ustawi wa kiuchumi kwa wateja wa Tigo.

“Ni matumaini yetu kuwa huduma hii itachochea utekelezaji wa lengo letu la kuwafikia wananchi kila kona ya nchi na zaidi kuchangia agenda ya ujumuishwaji wa watu kiuchumi.Kwa ushirikiano huu Tigo inakuza mtandao wake kwa kuwapa wateja njia mbadala ya kutoa fedha zilizoko kwenye akaunti ya Tigo Pesa kupitia ATM za UmojaSwitch.Hii inasaidiwa zaidi na mawakala zaidi ya 100,000 waliopo nchini,” amesema.

Amefafanua kuwa mteja wa Tigo atatakiwa kufuata hatua zifuatazo kwa ajili ya kuweza kutoa fedha kutoka katika ATM za benki ya UmojaSwitch, ambapo ata Piga *150*01, Chagua 7. Huduma za Kifedha, Chagua 5. Kutoa pesa ATM na ata chagua Benki, alafu ataandika Kiasi cha fedha anachotaka kutoa kisha namba yake ya siri.Katika ATM, mteja atabonyeza kitufe cha TigoPesa alafu ataingiza namba ya simu, kisha OTP(namba ya siri ya kutumika mara moja tu), halafu atapata fedha zake kutoka kwenye ATM.

Afisa Mkuu Mtendaji wa UmojaSwitch,Company Ltd, Danford Mbilinyi akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kuwa huduma hiyo mbali na kuongeza urahisi wa upatikanaji wa pesa pia itasaidia katika ukuzaji wa sekta ya fedha pamoja na kurahisisha ufanyaji wa miamala muda wowote.

Naye, Afisa Mkuu Mtendaji wa UmojaSwitch,Company Ltd, Danford Mbilinyi, alisema “ushirikiano huu utachochea ukuaji wa sekta ya fedha huku ukirahisisha upatikanaji wa huduma kwa watu wote kila mahali,” amesema.

Amesema UmojaSwitch ina farijika kushirikiana na Tigo ili kuwapatia wateja uhuru wa kifedha muda wote na zaidi kuokoa muda na gharama kwani ATM za UmojaSwitch zipo maeneo mengi ya nchi.

Habari Kubwa