Watendaji watiliwa shaka migogoro

05Dec 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
Watendaji watiliwa shaka migogoro

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Omar Kheir, amesema baadhi ya watendaji wanaoshughulika na masuala ya ardhi wanasababisha migogoro ya ardhi mijini na vijijini.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Omar Kheir.

Alisema kuwapo kwa migogoro hiyo kunasababisha wananchi kuilaumu serikali kwa kuona haiwatendei haki.

Hayo aliyaeleza wakati akifungua warsha kuhusu usimamizi, udhibiti na uendelezaji rasilimali ardhi visiwani humo.

Alisema, watendaji wengi wa sekta ya ardhi wanafanya kazi kwa mazoea kwa kutofuata sheria na utaratibu wa umiliki wa ardhi, hali inayosababisha migogoro ambayo wakati mwingine huiingiza serikali kwenye gharama.

"Vibali vinatolewa kiholela hata kwenye maeneo ya kilimo, vyanzo vya maji na sehemu za fukwe, hii ni hatari," alisema, Waziri Kheir.

Alisema wakati mwingine wanaibebesha gharama serikali kwa kuvunja maeneo yaliyovamiwa, hivyo aliwaonya watendaji hao kuachana na kadhia hiyo.

Alisema iwapo mtendaji yeyote atagundulika kuwa na tabia hiyo ambayo inasababisha migogoro ya ardhi atakatwa mshahara wake ili kulipia gharama za uvunjaji kwenye maeneo yaliovamiwa.

"Sitokuwa tayari kumuona mtendaji akifanya kinyume na utaratibu wa serikali kwenye umiliki wa ardhi, nitawashugulikia,” alisema.

 Aidha, aliwataka maofisa ardhi katika halmashauri, wilaya na mikoa kuwa waadilifu kwenye kutekeleza majukumu yao huku wakielewa ardhi ni mali ya serikali na ugawaji unakwenda kwa taratibu.

 

Waziri Kheir, alisema, ataendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kasi zaidi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Mazingira katika kuhakikisha matumizi ya ardhi yanafuata utaratibu.

"Watu wanaovunja sheria mbalimbali za ardhi kwa kujenga kwenye fukwe, sehemu za wazi, mahali pa watu wote, wajiandae," alisema.

Naye Waziri wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Mazingira, Salama Aboud Talib, aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kusimamia sheria, kuzitumia na kuzilinda kwa matumizi ya ardhi.

"Tulipofika hatuhitaji migogoro tena, iliyopita inatosha na hii tuliorithi tunaimalizia, hivyo nawaombeni tufungue ukurasa mpya ambao utatuletea tija sisi kama viongozi na kama serikali," alisema.

Aidha, alisema ardhi ni mali ya serikali inapotoa kumpa mtu, inampa kwa masharti na mikataba.

"Lakini tunajisahau na tunafanya kazi kwa mazoea na tumefika mahali yale yote tunayopanga ni kama tunatwanga maji kwenye kinu," alisema.

Hivyo, Waziri Salama, aliwataka watendaji kusimamia kwa vitendo yale yote yanayofikiwa kwenye maazimio ya kiutendaji badala ya kuwa na maneno yanakosa utekelezaji.