Watuhumiwa kujichukulia mkopo mil. 118/- kinyume cha sheria

07Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Hai
Nipashe
Watuhumiwa kujichukulia mkopo mil. 118/- kinyume cha sheria

MKUU wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Gelasius Byakanwa, ametoa amri ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka viongozi wa
Bodi ya Chama cha Akiba cha Kuweka na Kukopa cha Uswaa Mamba Saccos, wanaotuhumiwa kujiidhinishia kinyume cha sheria mkopo wa zaidi ya Sh. milioni 118.

Aidha, ameliagiza jeshi la polisi kukamilisha upelelezi wa tuhuma hizo ndani ya siku 30 na ihakikishe viongozi hao wanaburuzwa kortini kwa kusababisha wanachama 1,500 kukosa huduma hiyo.

Byakanwa alichukua uamuzi huo juzi, baada ya wanachama wa Sacoss hiyo kuituhumu bodi kukomba fedha zote na kukifanya chama kubakiwa na kiasi cha Sh. milioni 25, ambazo haziwezi kutosheleza mahitaji ya mikopo ya wanachama wake.

“OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) hakikisha viongozi wa bodi hiyo wanakamatwa na jalada la uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo linafunguliwa haraka. Lakini ndani ya siku 30 upelelezi uwe umekamilika na wapelekwe mahakamani,” aliagiza.

Kabla ya Byakanwa kuingilia kati sakata hilo, wanachama hao wa Uswaa Mamba Saccos, walinukuliwa na Nipashe wakilalamika kukosa fedha kutokana na viongozi waliotangulia wa bodi hiyo kuwatuhumu kuchukua fedha hizo.

“Ni jambo la kusikitisha kwa hatua waliochukua baadhi ya viongozi kujikopesha mamilioni ya shilingi bila kujali majaliwa ya chama hiki na wanachama wake. Walijiidhinishia fedha hizo kinyume na matakwa yetu na hadi leo hawajazirejesha,” alisema Gerald Mwanga.

Kwa upande wake, Elifinya Soka, alisema tangu vigogo hao walipojikopesha fedha hizo na kutozirejesha kwa muda mrefu sasa, mambo yamezidi kuwa magumu na yameanza kufuta malengo waliyokuwa wamejiwekea

Naye, Isaac Ulotu, akizungumza katika mkutano huo, alisema hali hiyo imewatia hasara kubwa kiuchumi hasa kutokana na wanachama wa Saccos hiyo kukosa mikopo ya kwa ajili ya shughuli za maendeleo kama vile kilimo, kusomesha watoto, ufugaji na ujenzi wa makazi.

Hivi karibuni, akitoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo, Meneja wa chama hicho, Shirilengwa Ulomi, alisema madai hayo yalianza mwaka 2013, baada ya viongozi wa bodi hiyo kujiidhinishia fedha hizo kinyume cha sheria, hali ambayo imesababisha shughuli za chama hicho kuanza kuzorota.

Habari Kubwa