Watuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha, wakamatwa mkutanoni

16Jan 2017
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Watuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha, wakamatwa mkutanoni

WAKAZI watatu wa Kijiji cha Kilosa Mpepo, tarafa ya Ngoheranga, Wilaya ya Malinyi, wamejikuta mikononi mwa polisi wakati wakihudhuria mkutano wa hadhara kati ya wananchi wa kijiji hicho na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Dk. Stephen Kebwe.

Wananchi hao walifika katika mkutano huo, wanadaiwa kufanya ubadhilifu wa fedha za michango ya ujenzi wa shule ya sekondari katika eneo hilo kiasi cha Shilingi milioni tatu na kusababisha kukwama kwa ujenzi.

Wakazi hao ni Athuman Lijola ambaye ni Mtendaji wa kata hiyo, Katibu wa ujenzi, Swadikina Maulid na Mhasibu wa kamati hiyo Ramadhan Hangahane, walijikuta katika dhahama hiyo, baada ya kudaiwa kuchangisha Sh. 17,500, kila kaya na fedha hizo kuzitumia kwa matumizi binafsi.

Katika mkutano huo, Dk. Kebwe alihoji sababu ya wananchi hao kushindwa kuendeleza ujenzi wa shule hiyo na kusababisha wanafunzi waliohitimu masomo ya msingi na kutakiwa kuendelea na sekondari, kulazimika kwenda kusomea katika kata nyingine mbali na kijiji hicho.

Baada ya maelezo hayo, walisimama wananchi hao, akiwamo Omar Hassan na kumueleza Dk. Kebwe kuwa viongozi hao walipita kuchangisha fedha kila kaya Sh. 17,500, baada ya wananchi kuhamasika, lakini mpaka sasa fedha hizo hazijulikani zilipo.

Amina Juma, mkazi wa kijiji hicho, alisema wanapouliza viongozi hao ujenzi huo kutoendelea, wakati wananchi wamechangishwa fedha, wamekuwa wakali na kuwatishia kuwaweka ndani.

Kufuatia malalamiko hayo, Dk. Kebwe, aliwamuru polisi aliofuatana nao, kuwakamata viongozi wa kamati hiyo, ili waende kutoa maelezo ya fedha za michango ya wananchi zilipo.

Dk. Kebwe, aliwataka wananchi wa Malinyi kuheshimu sheria zikiwamo ndogondogo, walizojiwekea za kusimamia na kutunza rasilimali zilizopo hususani ardhi na misitu ambayo kwa kiasi kikubwa ndio tegemeo kwa wananchi wengi.

Habari Kubwa