Watuma salamu Dodoma wapewa somo

23Mar 2019
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Watuma salamu Dodoma wapewa somo

WANACHAMA wa chama cha watuma salaam redioni mkoani Dodoma, wametakiwa kuchangamkia fursa za serikali kuhamia jijini hapo kujiinua kiuchumi badala ya kuishia kutuma salamu.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Mzee Langolango, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapo kuhusu maandalizi ya mkutano mkuu wao utakaofanyika Aprili 7, mwaka huu.

Alisema wanachama hao badala ya kujikita kwenye kutuma salamu ni wajibu wao pia kutumia nafasi zao katika fursa zilizopo za kiuchumi ambazo zitawawezesha kujiinua kiuchumi.

“Pamoja na watuma salamu kutoa elimu kwa kupitia tasnia ya habari, lakini wanatakiwa kujishughulisha na uwekezaji unaoweza kujipatia kipato cha kiuchumi badala ya kuishia kwenye kutuma salamu tu,” alisema.

Aidha, aliwasisitiza wanachama hao kuiunga mkono serikali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Uchumi wa viwanda vya kati ni kwa Watanzania wote, hivyo watuma salamu ni muhimu waiunge mkono serikali katika kuhakikisha azima hiyo inakamilika ila kwa kufanya kazi na kulipa kodi,” alisema.

Aliwataka kuibua miradi itakayowafanya kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.

Habari Kubwa