Watumiaji Tigo Pesa watangaziwa neema

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Watumiaji Tigo Pesa watangaziwa neema

KAMPUNI ya simu za mkononi  ya Tigo kupitia huduma yake ya Tigo Pesa,  imetangaza zawadi kwa wateja wake ambao watajishindia mamilioni ya pesa kupitia promosheni ya ‘fanya muamala na ushinde na Tigo Pesa’ inayoendeshwa katika msimu huu wa krismasi na mwaka mpya .

Ofisa Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo, Hussein Sayed.

Promosheni hiyo itakayodumu kwa kipindi cha mwezi mmoja, itashuhudia washindi watatu wa jumla wakijinyakulia Sh. milioni 15, milioni 10 na milioni tano kila mmoja. Pia kutakuwa na washindi wa kila siku ambao mmoja atashinda donge la Sh. milioni moja, huku wengine wanne wakijinyakulia Sh. 500,000 kila mmoja.

Ofisa Mkuu wa Huduma za Kifedha wa Tigo, Hussein Sayed, akizindua promosheni hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema wanatarajia kupata washindi 153 katika kipindi cha mwezi mmoja wa promosheni hiyo.

"Wateja watapata nafasi ya kushinda kwa kufanya miamala yoyote kutoka simu zao kupitia Tigo Pesa. Kadri unavyofanya miamala mingi zaidi ndivyo unavyojiongezea nafasi ya kushinda," alisema Sayed.

Alisema Tigo Pesa ni huduma ya fedha ya simu za mkononi ya pili kwa ukubwa nchini yenye mtandao mpana wa mawakala zaidi ya 70,000 waliosambaa kote nchini. Miamala ya takribani Sh. bilioni 1.7 hufanyika nchini kupitia Tigo Pesa kila mwezi.

Habari Kubwa