Wauza matunda watakiwa kuanza biashara saa 12

23Feb 2021
Julieth Mkireri
KIBAHA
Nipashe
Wauza matunda watakiwa kuanza biashara saa 12

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, ametoa agizo kwa wafanyabiashara wa matunda eneo la Mailimoja kuanza biashara saa 12, jioni na atakayekiuka hatua zichukuliwa dhidi yake.

Ndikilo alitoa agizo hilo juzi alipozungumza na  wafanyabiashara wa soko la Loliondo na soko jipya la Picha ya Ndege kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo la Mailimoja wanatakiwa kuanza saa 12 na muda mwingine waendelee katika soko la Loliondo.

"Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya mtende haki, anayetaka kufanya boashara ya matunda aanze saa 12 na si saa saba kama ilivyo sasa atakayekiuka mgambo kamata,” alisisitiza Ndikilo.

Kuhusiana na gharama za kodi zinazotozwa kwa skwea mita, alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji kukaa na uongozi wa wafanyabiashara hao kujadiliana namna ya kutatua kero zinazowabili.

Awali aliwasilisha kero za wafanyabiashara wa Loliondo Mwenyekiti wa soko hilo, Mohamed Mnembwe, aliomba kupunguzwa kwa gharama za kodi kwa mwezi ambazo wanatakiwa kutoa Sh. 8,000 ifike Sh. 3,000 ambayo wanna uwezo wa kuimudu.

Aidha, Mnembwe alisema uwapo wa kodi kubwa ya Sh. 8,000 imesababisha baadhi ya fremu kutotumika, na kwamba kati ya wafanyabiashara zaidi ya 338, ni 88 pekee wanaoendelea na biashara na zaidi ya 200 wamefunga fremu kwa kushindwa kulipia kodi.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jenifa Omolo, alisema suala hilo la kuomba kushushiwa kodi hadi Sh. 3,000 halikuwahi kumfikia ofisini kwake, na kwamba yuko tayari kukaa meza moja na uongozi wa soko kujadili kodi rafiki.

Solo la Loliondo lilianzishwa baada ya kuvunjwa kwa soko la Mailimoja ambalo lilikuwa kwenye hifadhi ya barabara, wafanyabiashara waligawiwa maeneo na kila mmoja alijenga kwa gharama zake kwa makubaliano na Halmashauri.

Kodi ya awali ilikuwa Sh.11, 000, lakini baada ya majadiliano ilishuka hadi Sh. 8,000, ingawa nayo inaelezwa kuwa kikwazo kwa baadhi ya wafanyabiashara kuendelea na biashara zao.

Habari Kubwa