Wauza shamba BoT isiifungie benki

17Jan 2018
Godfrey Mushi
Nipashe
Wauza shamba BoT isiifungie benki

CHAMA Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), kimejitwisha jukumu la kuinusuru Benki ya Ushirika ya KCBL isinyang'anywe leseni na kufungiwa na Benki Kuu (BoT),  kwa kuamua kuuza ekari 581 za Shamba la Lerongo.

KCBL inakabiliwa na upungufu wa mtaji, tatizo ambalo hualika BoT kunyang'anya leseni na kufungia benki husika, ikiwamo tano kwa pamoja mwanzoni mwa mwezi huu.

Aidha, benki hiyo ambayo inamilikiwa na KNCU kwa asilimia 69, inahitaji kiasi cha Sh. bilioni tano ili kufikisha mtaji wa Sh. bilioni 6.5 ulioelekezwa na BoT uwe umefikiwa hadi ifikapo Juni, mwaka huu.

Uamuzi wa kuuza shamba hilo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa KNCU, Aloyce Kitau, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa kuinusuru benki hiyo isifutiwe leseni.

“Baada ya kupokea taarifa juu ya upungufu wa mtaji wa kuendesha benki yetu ya ushirika, wanachama wa KNCU (1984) Ltd, waliridhia kuuza moja ya mali zake na fedha itakayopatikana iongezwe kwenye mtaji wa benki hiyo ili ifikie kiasi hitajika cha mtaji kama ilivyoelekezwa na Benki Kuu,” alisema Kitau.

Shamba la Lerongo lililowekwa sokoni kwa sasa na ambalo bado zabuni yake haijatangazwa hata hivyo, lipo katika wilaya ya Siha.

Kitau aliwasihi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kutumia benki hiyo kwani hadi kufikia jana michakato yote na kibali cha kuuza shamba hilo ilikua imekamilika, na kwamba KCBL itafikia mtaji husika kama inavyotakiwa kisheria mapema iwezekanavyo.

Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa kwa umma jana na makamu mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya KCBL, Tumaini Yarumba ilisema benki hiyo itatimiza vigezo vyote vya kuwa na mtaji hitajika kufikia Juni.Kwa mujibu wa Yarumba, Benki Kuu iliitaka KCBL kuhakikisha inaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote wa mkoa wa Kilimanjaro. 

Taarifa hiyo inakwenda sambamba na tangazo la BoT la Januari 9, mwaka huu linalotaka wananchi kuwa na imani kwa sekta ya kibenki nchini kuwa iko imara na tayari kuwahudumia Watanzania wote kwa ukaribu.

Akitoa ufafanuzi kuhusu umiliki wa benki hiyo, Meneja wa KCBL, Joseph Kingazi alisema benki hiyo ya ushirika ina wanahisa 245 ambao ni Vyama vya Ushirika wa Mazao (Amcos), Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (Saccos) pamoja na watu binafsi.

KCBL iliyoanzishwa miaka 20 iliyopita, ndiyo benki ya kwanza ya ushirika nchini kufunguliwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na ndio waanzilishi wa mfumo wa stakabadhi ghalani.

BENKI TANOJanuari 4 BoT ilizifungia na kusitisha shughuli za benki tano zilizokuwa zinafanyabiashara zake nchini baada ya kushindwa kutimiza matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Gavana mstaafu wa BoT, Prof. Benno Ndulu alitangaza kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kuzifunga Covenant Bank for Woman, Benki ya Efatha, Njombe Community Bank, Benki ya Kagera na Meru Community Bank baada ya kuzifutia leseni na kuziweka chini ya mfilisi.

Benki hizo zilifungwa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mtaji na nyingine tatu, ikiwemo KCBL kuwekwa kwenye uangalizi wa miezi sita mpaka Juni.

Benki mbili nyingine zinazokabiliwa na hali kama ya KCBL ni Benki ya Wanawake (TWB) na Tandahimba Community Bank.

“Kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu Na. 41(a) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006; Benki Kuu ya Tanzania imeiteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa mfilisi kuanzia tarehe 04 Januari 2018,” ilisema taarifa hiyo ya Prof. Ndulu.

Taarifa ilisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya BoT kujiridhisha kuwa benki hizo zina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya Sheria na kanuni zake. 

"Upungufu huo wa mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na kwamba kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki hizo kunahatarisha usalama wa amana za wateja wake.”

Taarifa hiyo iliuhakikishia umma kuwa Benki Kuu ingeendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta uhimilivu katika sekta ya fedha. 

Habari Kubwa