Wauzaji ramani kiholela washukiwa

04Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wauzaji ramani kiholela washukiwa

 

BODI ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), imewataka wafanyabiashara wa ramani za majengo nchini kuacha kuuza ramani hizo mara moja kwani zimekuwa ni chanzo kikubwa cha ujenzi holela usiozingatia viwango vya ubora.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Ludigija Bulamile.

Bodi hiyo imesema kumekuwa na matatizo ya kuporomoka kwa majengo, nyumba kuwa na nyufa pamoja na ujenzi unaoziba miundombinu mingine.

Kwamba hali inayotokana na wenye nyumba wengi kutofuata sheria za ujenzi pamoja na viwango vya ubora.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dk. Ludigija Bulamile, alisema watu wanaouza ramani hawaangalii wala kupima viwango vya ujenzi unaotakiwa mahali husika maana wataalamu wa masuala hayo kabla ya kukushauri aina ya jengo linalohitajika kutokana na hali ya udongo.

“Wauza ramani wote wa nchini muache mara moja kuuza ramani hizo, hamna utaalamu wa kumshauri mtu kuhusiana na jengo linalohusika, mnauza ramani ovyo watu nao wananunua tu, hii inasababisha nyumba nyingi kupata ufa na kubomoka hii inahatarisha maisha ya watu,” alisema Dk. Lidigija.

Alisema kuna maeneo hayaruhusiwi kujenga nyumba za ghorofa au nyumba kubwa kutokana na ardhi iliyopo, na wakati mwingine ardhi inakuwa na maji, hivyo kuhitaji msingi mkubwa na mchanganyiko wa zege imara. Lakini watu wananunua na kujenga kwenye maeneo hayo bila kuzingatia athari zinazoweza kutokea.

“Nawashauri wakati wa kujenga mtumie wataalamu waliosomea fani ya ubunifu na ukadiriaji majenzi ili kuepukana na hasara ya kujenga nyumba mara mbili, unajua usipotumia wataalamu hawa eti unasema unaokoa gharama matokeo yake unajikuta unatumia gharama mara mbili zaidi kwani yanabomoka, au wanapindisha nyumba, hawazingatii viwango na mchangayiko mzuri wa nyenzo za ujenzi,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dk. Geraldine Kikwasi, alisema wakadiriaji majenzi wamekuwa na mchango mkubwa wa kuhakikisha majengo yanakuwa imara na hivyo kuwaomba Watanzania kuwatumia ili kuimarisha sekta hiyo.

“Wakadiriaji majenzi ni watu muhimu sana, ni muhimu kuwatumia, nashauri halmashauri zote kuajiri watu hawa ili kupangilia miji yetu na majengo kwa ujumla,” alisema Dk. Kikwasi.

Naye mbunifu majengo ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi hiyo, Mbaraka Igangula, alisema utafiti uliofanywa na bodi hiyo hivi karibuni umebaini kuwapo kwa zaidi ya asilimia 90 ya makazi jijini Dar es Salaam kutokuwa na ubora kutokana na kutotumia wataalamu wa ujenzi katika kujenga makazi yao.

Alisema kuanzia sasa watahakikisha majengo makubwa yote nchini yanajengwa kwa kufuata sheria za ujenzi ikiwamo kutumia wataalamu wa ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi ili kujenga majengo imara.

Albert Munuo ni Kaimu Msajili wa AQRB, alisema wataalamu hao hivi sasa ni wachache nchini, hivyo kuwaomba wanafunzi wengi zaidi kusomea fani hiyo ili kuongeza wataalamu katika sekta hiyo.

Habari Kubwa