Wavuvi kicheko kuanzishwa wizara ya uchumi wa buluu

21Nov 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wavuvi kicheko kuanzishwa wizara ya uchumi wa buluu

SIKU moja baada ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kuunda Baraza la Mawaziri, wadau wa uvuvi wamepongeza kuazishwa kwa wizara mpya ya uchumi wa bluu na uvuvi.

Wakizungumza jana na Nipashe kwa nyakati tofauti, wadau hao walipongeza hatua ya Rais Mwinyi ya kuunda wizara hiyo hali inayoonyesha kwamba serikali ya awamu ya nane imepania kuendeleza sekta ya uvuvi ili kuinua uchumi wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo wa Wavuvi wa Kojani, Omar Muhammed Ali, alisema anampongeza Dk. Mwinyi kwa kuonyesha juhudi za kuboresha sekta ya uvuvi kutokana na ukweli kwamba kijiografia Zanzibar imezungukwa na bahari na wananchi wake wanategemea uvuvi.
 
Alisema wakazi wengi wa Zanzibar wanategemea bahari kama sehemu ya kimbilio salama, hivyo kuanzishwa na wizara hiyo ni jambo jema na wako tayari kutoa ushirikiano kwa serikali.
 
Hata hivyo, alishauri watendaji watakaopewa dhamana akiwamo waziri wa wizara hiyo, wajue wana wajibu wa kusimamia majukumu ya kuendeleza uvuvi na kuwa karibu sana na wavuvi.
 
Aliomba kuwekwe mazingira rafiki ambayo yatatekelezeka baina ya waliopewa dhamana ya kusimamia wizara hiyo na wavuvi wenyewe.
 
“Tunaomba kuwe na vikao vya mara kwa mara kubadilishana mawazo, kupitiwa kwa Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2010 ambayo imetoa mamlaka ya kudhiti maeneo ya bahari,” alisema.
 
Naye Ofisa Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Muhammed Khamis Mwamvura, alisema wizara hiyo mpya ina muono mkubwa na italeta manufaa kwa Zanzibar kwa sababu uchumi wa buluu si uvuvi pekee bali hata utalii, hivyo Zanzibar itakua kiuchumi.
 
Alisema kuwa hata Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli, alisema atanunua meli nane za uvuvi wa bahari kuu ambazo kati ya hizo nne zitaletwa Zanzibar, hivyo uchumi wa buluu utaleta neema kubwa.
Muhammed alisema Rais Mwinyi katika kampeni zake alisema atajenga bahari ya uvuvi, hivyo pia viwanda vya kuchakata samaki vitajengwa na Wazanzibari watanufaika kupitia mazao ya baharini.
 
“Wizara hii ya uchumi wa buluu na uvuvi ni wizara mama kulingana na sera ya Rais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi, ambayo ameipa kipaumbele,” alisema.
 
Katibu wa Ushirika wa Wakulima Hai unaoshughulika na Majongoo Bahari Zanzibar, Semeni Mohammed, alisema ukulima wa majongoo una faida kubwa, hivyo kuanzishwa kwa wizara hiyo kutasaidia kutatua kwa matatizo katika ufugaji huo.
 
Alisema hakuna mazingira rafiki katika shughuli hiyo hasa katika usafirishaji wa majongoo bahari nje ya nchi ambako yana soko kubwa duniani hasa nchini China.
 
“Tunataka tutambulike kuwa ufugaji wa majongoo bahari na ni moja ya uchumi ambao utatoa ajira nyingi kwa watu wa ukanda wa pwani hasa ikizingatiwa soko lake ni kubwa na wateja wanatusubiri kupeleka bidhaa zetu,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uvuvi Zanzibar (ZAFICO), Zahor Kassim, alisema anapongeza kuanzishwa kwa wizara hiyo na kwamba shirika lake lina miradi mbalimbali ya kuendeleza uvuvi ikiwama kujenga kiwanda cha kuchakata dagaa na samaki.
 
Alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 20 za samaki kwa siku na kitakuwa na eneo la kuhifadhi tani 1,500 za samaki.
 
Pia alisema sehemu kubwa ya uchumi wa buluu ni uvuvi hivyo kuazishwa kwa wizara hiyo kutasaidia kuendeleza miradi yao.

Habari Kubwa