Wavuvi wafunguka kukosa mikopo

03Jul 2019
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Wavuvi wafunguka kukosa mikopo

CHAMA cha Ushirika cha Wavuvi Tanzania (Chakuwata) kimesema kutokana na wavuvi kutoaminiwa na taasisi za fedha, kunachangia raia kutoka mataifa mengine kuwekeza na kunufaika na sekta hiyo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Rigoberth Mpemba, alisema hayo jana katika hafla ya kutia saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kati yao na Benki ya Posta Tanzania (TPB), jijini hapa.

Alisema wanashindwa kushiriki kwenye uchumi wa viwanda kutokana na vipato duni kwa kuwa hawajaaminiwa na taasisi za fedha.

Mpemba alibainisha kuwa raia wa kigeni wamekuwa wakiwekeza na kufaidika na rasilimali za uvuvi huku wazawa kwenye sekta hiyo uchumi wao ukiwa duni.

Aidha, alisema chama hicho kinaundwa na vyama vidogo 24 vyenye wanachama 2,500 katika mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Pwani, Kigoma, Mwanza, Tanga na Rukwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa TPB, Sabasaba Moshingi, aliwashauri wavuvi kujiunga katika vikundi ili kusaidiwa mikopo yenye masharti nafuu na taasisi za kifedha itakayowawezesha kununua vitendea kazi na kuinua uchumi wao.

Alisema madhumuni ya akaunti hiyo ni kuwawezesha wadau wa sekta ya uvuvi kujiwekea akiba  ili kunufaika na huduma za kifedha.

Alitaja lengo lingine la kuanzisha akaunti hiyo kuwa ni kutoa fursa ya kukuza shughuli za uvuvi.

Naye, Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Sadick Chikula, alikitaka chama hicho kufungua matawi kwenye mikoa yote yenye shughuli za uvuvi ili kuwa na uwakilishi mpana na kutambulika na mamlaka zingine.