Wavuvi walia na sheria ya usajili

23Oct 2019
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
Wavuvi walia na sheria ya usajili

WAVUVI na wadau wa sekta hiyo wameiomba serikali kubadili sheria ya kusajili, kuanzisha na kufungua akaunti kwa ajili ya vyama vya ushirika wa wavuvi.

Aidha, walisema wanaomba wapatiwe washauri pamoja na watalaamu wa kuwashauri kwenye miradi mbalimbali na kuitaka serikali pia iwahimize watendaji wa ushirika kuacha kukaa ofisini na badala yake wawafuate wavuvi katika maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kuwapatia elimu ushirika.

Ombi hilo lilitolewa na wanachama wa Butuja Saccos ambao ni wavuvi wa ndoano wa mwalo wa Butuja uliopo wilayani Ilemela mkoani Mwanza wakati wakizungumza na Nipashe jijini hapa.

Katibu wa Butuja Saccos na Mwenyekiti wa vikundi vya usimamizi na ulinzi wa rasilimali za uvuvi (BMU) Butuja, Dickson Maila, alisema wana nia ya kuanzisha na kusajili chama chao cha ushirika lakini changamoto ni sheria yake ambayo inawataka kuwa na milioni tano hivyo kuiomba serikali kabadili sheria hiyo.

"Tuna nia ya kuunda ushirika wa wavuvi Butuja ila sheria ya ushirika ambayo inatutaka ili tusajili chama na kufungua akaunti ni lazima tuwe na Sh. milioni 5.0”

Alisema maelekezo hayo waliyapata kutoka kwa Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Ilemela hivyo hawajui kama ni kweli au aliwapiga changa la macho kwa vile yeye ni mtaalamu wa serikali hivyo kuwalazimu kuyafuata.

Aliongeza kuwa, fedha hiyo wameanza kuitafuta sasa ni mwaka, hivyo wakashauri ngazi husika kurekebisha sheria ya ushirika hata kama chama kitakuwa na milioni mbili kisajiliwe.

Alisema kama ingekuwa kusajili ni milioni mbili hata Butuja wangesajili na wameanza mchakato wa kutafuta hiyo milioni tano ili wasajili.

Alisema, ili wavuvi wahamasike kuanzisha na kusajili vyama vya ushirika katika maeneo yao hususani wanaotumia ndoano elimu juu ya ushirika inapaswa kutolewa na wataalamu hao.

"Shida ni elimu kwani wataalamu wa ushirika wanakaa zaidi ofisini nakusahau kuja kutoa elimu kwa wananchi wenye adhima za kujiinua kiuchumi," alisema.

Katibu wa BMU ya Butuja, Emmanuel Nyagwesi, alisema katiba imekamilika wanachosubiri ni kuipeleka kwa mwanasheria kabla ya kuiidhinisha kisha wasajili ushirika wao muda wowote kuanzia sasa.

"Tunaomba tukishasajili ushirika wetu tuelekezwe ni wapi serikali itakuwa imetuwekea mkono yaani ni benki gani na sehemu ipi ambayo itaweza kutupatia mkopo kwani shida ni mtaji tukipata fedha tutapanua wigo wa biashara.”

Kaimu Mwenyekiti wa Butuja Saccos, Khamisi Ramadhani, aliiomba, serikali iwaangalie kwa jicho la pili na iwasaidie kwa kuwaagiza walimu, wanao husika na ushirika wawatembelee.

Habari Kubwa