Wawakilishi sasa wataka kuimarisha mazao ya viungo

23Feb 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wawakilishi sasa wataka kuimarisha mazao ya viungo

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, kuimarisha kilimo cha mazao ya viungo.

Wajumbe hao wamesema uzalishaji wa mazao hayo umeshuka na unachangia wakulima kukosa mapato.

Hayo yalisemwa na mwakilishi wa jimbo la Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja, Sulubu Kidongo Amour, wakati akichangia mwelekeo wa hali ya uchumi, mpango wa maendeleo na bajeti kwa mwaka 2021/22 na 2023/2024.

Alisema kilimo cha mazao kilichokuwa maarufu kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja cha Tangawizi pamoja na Manjano hivi sasa uzalishaji wake umeshuka kwa kiwango kikubwa.

Alisema wakulima wengi wa kilimo hicho ambao ni wazawa wameacha kulima kutokana na wizara kushindwa kuwashawishi wakulima pamoja na kuwapa elimu.

''Kilimo cha viungo cha tangawizi na manjano hivi sasa kimeanza kupotea Zanzibar kwa sababu wizara yetu imeshindwa kuwahamasisha wakulima pamoja na kuwapatia elimu na utaalamu,” alisema Amour.

Mwakilishi wa jimbo la Konde, Zawadi Amour Nassor, alisema kilimo cha mazao ya viungo ni muhimu kwa sababu kwa sasa soko lake la nje ya nchi ni la uhakika.

Hata hivyo, alizitaka taasisi na wizara husika kuwahamasisha wakulima kulima kilimo hicho ambacho kina uhakika wa kupata fedha na soko.

Mwakilishi wa viti maalumu wanawake, Mwantatu Mbarouk Khamis, alisema pamoja na sekta ya kilimo kupewa kipaumbele na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini bado haijaleta tija na mabadiliko kwa wakulima vijijini.

Alisema miaka ya nyuma Zanzibar ilikuwa maarufu katika ukanda wa Afrika  Mashariki kwa uzalishaji wa mazao ya viungo na soko kwa nchi za Ulaya na mashariki ya mbali hadi Asia, na kwamba kuna haja ya kukipigania.

''Tunaiomba wizara ya kilimo kuwahamasiaha wakulima wetu wa vijijini na kuwapatia elimu na mbinu za kilimo bora cha mazao ya viungo',”alisema Khamis. 

Habari Kubwa