Wawakilishi walilia sera ajira kubana wawekezaji

23May 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Wawakilishi walilia sera ajira kubana wawekezaji

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameitaka serikali kutayarisha sera ya ajira ambayo itakuwa mwongozo na kuwabana wawekezaji wa kigeni na kuwalazimisha kuajiri wafanyakazi wazalendo nchini.

Mwakilishi wa Shauri Moyo, Hamza Hassan Juma, aliyasema hayo wakati akichangia bajeti ya makadirio mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Mambo ya Kale kwa mwaka 2019-2020.

Juma alisema hakuna sera ya ajira ambayo inawaelekeza wawekezaji wa nje kuajiri wafanyakazi wazalendo katika sekta mbalimbali ikiwamo hoteli za kitalii.

Alisema hoteli nyingi za kitalii zimeajiri wafanyakazi wa kigeni kwa visingizio mbalimbali ikiwamo hakuna wafanyakazi wazalendo wenye sifa.

''Tunapiga kelele sana katika suala la ajira kwa wafanyakazi wetu wazalendo katika sekta za hoteli za kitalii...njia pekee ya kudhibiti na kukabiliana na tatizo hilo ni kutunga sera itakayowabana wawekezaji hao kuajiri wafanyakazi wazalendo,” alisema.

Naye Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, alisema wapo wawekezaji wengi wa nje ambao hawatoi kipaumbele cha ajira kwa wafanyakazi wazalendo.

Alisema njia pekee ya kuwabana ni kuweka sheria madhubuti na kuhakikisha wafanyakazi wazalendo wanapata ajira.

Alieleza zipo baadhi ya nchi ambazo mwwekezaji anapokwenda kuwekeza anapewa masharti ikiwamo kuhakikisha asilimia fulani ya ajira zinakwenda kwa wazalendo.

“Sasa wakati umefika tuhakikishe kwamba tunatunga sera zitakazowabana wawekezaji wanaokuja kutoa ajira kwa wafanyakazi wazalendo ili wafaidike na sekta ya uwekezaji,” alisema.

Mwakilishi wa Chaani, Nadir Abdulatif Yussuf, aliwapongeza wawekezaji wazalendo aliwamo Mwenyekiti wa makampuni ya Azam, Said Salim Bakhresa, kwa kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wafanyakazi wazalendo katika kampuni zake.

Alisema Bakhresa ameajiri sehemu kubwa ya wafanyakazi kutoka Zanzibar, hivyo wazalendo kufaidika na uwekezaji wake.