Wawekezaji kunyang’anywa mashamba

27Jun 2017
Steven William
MUHEZA
Nipashe
Wawekezaji kunyang’anywa mashamba

SERIKALI mkoani Tanga imewaonya wawekezaji wakubwa ambao walichukua mashamba ya mkonge na kushindwa kuyaendeleza kuwa yatachukuliwa na serikali na kupewa wananchi walime.

Mkuu wa mkoa wa tanga, Martin Shigella.

Onyo hilo lilitolewa na Mkuu wa mkoa huo, Martin Shigella, wakati wa kupokea taarifa ya Wilaya ya Muheza ambayo ilisomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Luiza Mlelwa.

Alisema kuna watu wanaojifanya wawekezaji wa kilimo kikiwamo cha mkonge wamechukua mashamba makubwa kwa lengo la shughuli za kilimo, lakini wameyatelekeza badala ya kuyaendelea, hivyo wananchi kukosa maeneo ya kulima.

Shigella alisema kutokana na hali hiyo, ameagiza wawekezaji wote waliyochukua mashamba hayo bila kuyaendelea yakiwamo ya mkonge wayarudishe mara moja serikalini ili wapewe wananchi walime na kwamba hilo ni agizo la Rais John Magufuli, kwani hawataki kuona mwekezaji amefuga pori huku wananchi wakipata shida ya mashamba ya kulima.

Aliwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanawafuatilia wawekezaji ambao wenye mashamba waliyopewa na serikali, lakini hawayaendelezi watoe taarifa mkoani ili mashamba hayo yachukuliwe wananchi.

Katika hatua nyingine, Shigella alisema kuwa shule nyingi zina wanafunzi hewa, lakini zinapelekewa fedha za maendeleo na kwamba walimu wakuu wanazitumia.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliwaagiza wakuu wa shule hizo kuorodhesha idadi ya wanafunzi katika shule zao na kupeleka kwa waratibu wa elimu kata ambao nao watapeleka kwa ofisa elimu wilaya ambaye atawasilisha taarifa kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Alisema baada ya hapo naye atapeleka idadi hiyo kwa mkuu wa wilaya na mkuu wa wilaya atapeleka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tanga na wao watapeleka Taifa.

Shigella alitoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa vyumba  vitatu  vipya vya madarasa  katika Shule ya Msingi Kiwanda Kata ya Tongwe wilayani Muheza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Luiza Mlelwa, alisema shule za msingi na sekondari zinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu, hivyo kuomba waongezewe walimu.

Habari Kubwa