Wawekezaji wahakikishiwa mazingira rafiki

29Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe
Wawekezaji wahakikishiwa mazingira rafiki

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji ), Angela Kairuki, amewahakikishia wawekezaji wenye viwanda Nyanda ya Juu Kusini kuwa serikali inashughulikia changamoto mbalimbali.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji ), Angela Kairuki:PICHA NA MTANDAO

Miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni kwa nishati na miundombinu mingine ya uhakika lengo likiwa kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Sambamba na hilo, Waziri Kairiki amesema serikali ambayo imeazimia kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025,  ilishachukua hatua mbalimbali muhimu kuweka mazingira mazuri yatakayovutia uwekezaji.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kuhitimisha ziara yake katika ushoroba wa kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kwa kutembelea viwanda vya Tukuyu Srings Water, Raphael Group Limited, Stawisha (Dutch Potato Project), Tanzania Breweries Limited ( TBL) na Marmo Granito Mine ( T) Ltd, Kairuki, alisema serikali inatambua umuhimu wa uwekezaji katika kuinua uchumi.

“Ninawapongeza kwa uwekezaji huu wenye uhakiki na kwa upande wa Serikali tutaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Kwa upande wa serikali imeshachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa mazingira ya kuwekeza yanaendelea kuwa rafiki,” alisema.

Aliipongeza SAGCOT kwa kushirikiana na wadau wake kwa kazi nzuri wanayofanya katika katika ushoroba huo kuhakikisha wanaboresha na kuwajengea uwezo wakulima wadogo na kati kwa kuwafundisha mbinu za kilimo chenye tija ambacho kimekuwa na matokeo chanya katika kujikwamua kiuchumi na kuchochea uwekezaji eneo hilo.

Waziri alisema kuwapo kwa Ofisi ya Kanda ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) katika mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa hatua thabiti serikali

imekuwa ikizichukua kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapata huduma kwa karibu zaidi.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Raphael Group Limited, kinachojihusisha kuongeza thamani ya mazao ya nafaka,  Raphael Ndelwa, aliipongeza SAGCOT kwa kuwafungulia njia ya kibiashara kwa kuwaunganisha na taasisi za kilimo pamoja na kukidhi mahitaji ya kiwanda.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Stawisha linalojihusisha na kilimo cha viazi mviringo,  Theresia Mcha, alisema shirika lao linafanya

kazi kwa ukaribu sana na wakulima wa viazi mviringo na kuhimiza kilimo bora cha viazi na kuongeza tija.

Habari Kubwa