Wazabuni sasa waamua kumkimbilia Magufuli

08Mar 2017
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wazabuni sasa waamua kumkimbilia Magufuli

CHAMA cha wazabuni mkoa wa Mbeya (Chawambe) kinakusudia kuzishitaki kwa Rais John Magufuli taasisi za serikali zilizohudumiwa na kushindwa kufanya malipo kwa muda mrefu.

rais john magufuli.

Chawambe inadai kutoa huduma mbalimbali kwenye taasisi hizo, ikiwemo dawa na vifaa tiba kwa hospitali, chakula kwa shule za sekondari na huduma za ulinzi bila kulipwa kwa muda mrefu.

Wakizungumza na wandishi wa habari juzi mkoani hapa, wazabuni hao walisema wameamua kumlilia Rais baada ya kufuatilia malipo yao kwa muda mrefu kupitia ngazi mbalimbali bila mafanikio.

Mwenyekiti wa chama hicho, Mustafa Ngonyani alisema taasisi hizo kwa ujumla zinadaiwa na wazabuni hao zaidi ya sh. bilioni tatu tangu mwaka 2011, na kwamba Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya pekee inadaiwa zaidi ya sh. bilioni moja.

Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni Jeshi la Magereza linalodaiwa zaidi ya sh. milioni 300, vyuo vya kilimo ambavyo ni Uyole, Igurusi na Chuo cha Kilimo Inyala ambavyo kwa ujumla vinadaiwa zaidi ya sh. milioni 400 na Chuo cha Ustawi wa Jamii cha Ilambo ambacho kinadaiwa sh. milioni 50.

Ngonyani alizitaja taasisi za elimu zinazodaiwa kuwa ni Shule ya Wasichana Loleza, Shule ya Ufundi Stadi ya Wavulana Iyunga, shule ya wasichana ya Kayuki, shule ya Kutwa ya Mbeya na shule ya Kutwa ya Tukuyu.

“Tumejaribu kudai fedha hizo kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeshindikana, tumefuatilia kwenye Ofisi za Wizara husika hatujafanikiwa hivyo tumeamua tuende kwa Waziri Mkuu ambaye tuna imani atatusaidia, lakini kama itashindikana tutaenda mpaka kwa Rais Magufuli,” alisema Ngonyani.

Ngonyani aliongeza kuwa walifuatilia mpaka kwenye Ofisi ya Kamishna wa Bajeti katika Wizara ya Fedha na Mipango na wakaahidiwa kuwa wangelipwa sehemu ya fedha hizo mwezi Januari, lakini mpaka sasa hawajalipwa.

Naye Michael Ukway, ambaye ni miongoni mwa wazabuni hao, alisema anaidai Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe sh. milioni 200 ambazo kwa muda mrefu hajalipwa.

Alisema wakati wanafuatilia madeni hayo kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, alijibiwa na Katibu Tawala wa Mkoa kuwa Halmashauri hiyo haina fedha hivyo inaomba iwe inalipa sh. milioni tano kwa awamu, kiasi ambacho alidai ni kidogo.

Ukway alisema baadhi ya wazabuni hao wameingia hasara kwa mali zao kutaifishwa na taasisi za kifedha ambazo walikopa fedha hizo, hivyo akaiomba serikali kuwasaidia ili walipwe na ikiwezekana waendelee kutoa huduma.

“Kuna baadhi ya wenzetu walikopa mitaji kwenye taasisi za fedha wakiamini wangerejesha baada ya kulipwa na serikali, lakini mpaka sasa hawakulipwa na hivyo zile taasisi ziliuza nyumba zao, magari na mali zingine," alisema Ukway.

"Sasa tunamuomba Rais wetu atusikie kilio chetu maana Wizara ya Ujenzi aliyokuwa anaiongoza kabla hajawa rais haidaiwi kitu na wazabuni.”

Alisema hali inakuwa mbaya kutokana na fedha wanazokopa kwenye taasisi za fedha kuzirejesha kwa riba wakati madeni wanayozidai taasisi za serikali hayana riba.

Jokate afundisha ujasiriamali sekondari

Na Mwandishi wetu

Mrembo Jokate Mwegelo ameanzisha mpango maalum wa kufundisha somo la ujasiriamali kwa wanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari ya Majani ya Chai iliyopo Vingunguti katika Manispaa ya Ilala.
Jokate ataanza mafunzo hayo maalum kwa wanafunzi wa kike kuanzia wiki ijayo lengo likiwa ni kuwapa ufahamu wanafunzi hao wa kuanzisha biashara zao, mara baada ya kumaliza elimu yao ya sekondari.
Alisema kuwa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi ni muhimu kwani yanawawezesha kujiandaa vizuri kukabiliana na maisha, mara baada ya kuhitimu masomo yao ya sekondari na kushindwa kuendelea na masomo ya ngazi ya juu.
Kwa mujibu wa Jokate, mwanafunzi anaweza kusoma mpaka Chuo Kikuu ndani na nje ya nchi, lakini akakabiliana na ugumu wa kupata ajira ambazo kwa sasa ni haba.
“Kuna wengine wamesomea taaluma fulani kwa ngazi ya Chuo Kikuu lakini mpaka sasa hawana ajira na kukata tamaa katika maisha," alisema. Pia unaweza kufanya kazi tofauti na taaluma uliyosomea."
"Lakini kwa ujasiriamali ni tofauti, utajifunza jinsi ya kupata mtaji, kukopa na kurejesha, kufanya biashara gani na mbinu zake.
“Mfano halisi mimi mwenyewe, nimesomea mambo tofauti na kazi ninazozifanya ni tofauti, ni mbunifu wa mitindo, mavazi, muigizaji wa filamu, mwanamuziki na pia ni mfanyabiashara.
"Haya yote sikusomea, ila najivunia kwani ndiyo yanaendesha maisha yangu, wanafunzi wana vipawa tofauti, naamini katika programu hii nitapata wengi na kupata mafanikio.”
Alisema atakuwa anafundisha mafunzo hayo mara moja kwa wiki.
“Nimeamua kuanza rasmi siku ya wanawake duniani, maandalizi yamekamilika na nawaomba wanafunzi wajiandae kwani mafunzo ni mazuri na yatawajengea moyo wa kujiamini kwani si kila anayesoma anatakiwa kuajiriwa.”

Habari Kubwa