Wazalishaji, wasindikaji mafuta wapewa angalizo

22Feb 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wazalishaji, wasindikaji mafuta wapewa angalizo

WASINDIKAJI na wazalishaji wa mafuta ya kupikia, wameshauriwa kuacha tabia ya kuuza bidhaa hiyo wakiwa wameianika juani kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria za viwango.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango nchini (TBS), Hamis Mwanasala, alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo maalumu kwa wasindikaji, wafanyabiashara wa mafuta na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Alisema kitendo cha kuanika mafuta hayo juani kinasababisha bidhaa hiyo kupoteza ubora na kuhatarisha afya za watumiaji kutokana na baadhi ya virutubishi muhimu kupotea.

Vilevile aliwataka wadau hao kuandaa bidhaa hiyo katika mazingira ya usafi ili kulinda afya za watumiaji kwa madai kuwa watumiaji wa bidhaa hiyo nchini ni wengi.

“Lakini pia kwenye mafunzo haya tutatoa elimu juu ya ufungashaji bora na uwekaji wa taarifa muhimu kwenye vifungashio, usajili wa bidhaa na majengo ya kuzalishia na kuhifadhia, baadhi ya kazi hizi awali zilikuwa zinafanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na vifaa tiba (TMDA),” alisema Mwanasala.

Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, alisema wanaendesha mafunzo hayo katika mikoa mbalimbali nchini, lakini kwa Nyanda za Juu Kusini wameanzia katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Songwe.

Alisema mafunzo hayo yanagharamiwa na Serikali, hivyo washiriki wanafundishwa bure, na kwamba kwa Mkoa wa Mbeya watatoa mafunzo hayo katika wilaya za Mbeya, Rungwe, Kyela, Chunya na Mbarali ambapo kila kituo kitakuwa na washiriki 80.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwalinda watumiaji wa bidhaa hiyo wasipate madhara kwa kuhakikisha wazalishaji wanazingatia usafi kuanzia kwenye uzalishaji mpaka kwenye uhifadhi.

Andusamile alisema mafuta ni bidaa muhimu ambayo inatakiwa kutunzwa vizuri na kwamba wazalishaji na wadau wengine wanatakiwa kushiriki kwenye mafunzo ili elimu hiyo isambae kwa watu wengine.

“Sisi kama wasimamizi tumeona ni muhimu kuonana na hawa wadau ili wapate elimu, sasa tunawataka hawa wachache waliohudhuria mafunzo haya kwenda kuwa mabalozi huko mitaani kwa kuwaelimisha wenzao,” alisema Andusamile.

Alisema kuna baadhi ya maeneo mafuta huwa yanaonekana kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu hata bila kuyapima kwenye maabara hivyo akawataka wasindikaji kubadilika.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Noah Mkasanga, alisema sera ya nchi kwa sasa inasisitiza kuongeza usindikaji wa mazao mbalimbali na kwamba miongoni mwa mazao hayo ni mbegu za mafuta.

Alisema mbali na wasindikaji na wafanyabiashara hao kupatiwa mafunzo ya kuzingatia ubora wa bidhaa pia wanafundishwa sera mbalimbali za nchi pamoja na matakwa ya soko la kimataifa ili wasitegemee soko la ndani pekee.

Nao baadhi ya wasindikaji wa mafuta walisema bei ya bidhaa hiyo imepanda kwa kiwango kikubwa kutokana na uhaba wa alizeti uliosababishwa na mvua iliyonyesha kupita kiasi msimu uliopita.

Katika mafunzo hayo pia walihudhuria maofisa mbalimbali wakiwamo maofisa kutoka katika Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Habari Kubwa