Wazazi wameonywa kutumia fursa mimba za utotoni kujipatia mali

04May 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wazazi wameonywa kutumia fursa mimba za utotoni kujipatia mali

WAZAZI mkoani Shinyanga, wameonywa tabia ya kutumia kesi za mimba za utotoni kumaliza kesi kimya kimya na upande wa mtuhumiwa, kwa kupewa pesa ama mifugo, na kusababisha wahalifu kutofungwa jela.

Katibu wa Shirika la YWCA Marysiana Makundi, akizungumza kwenye kikao cha kujadili na kupanga mikakati ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

 

Imeelezwa kuwa hali hiyo inachochea vitendo hivyo kuendelea ndani ya jamii hasa mkoani humo na kuzima ndoto za wanafunzi wa kike.

Katibu wa Shirika la YWCA, Marysiana Makundi, amebainisha hayo leo kwenye kikao chao na wajumbe wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya Kata ya Ibadakuli ambayo wanatekeleza mradi wa kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Amesema baadhi ya wazazi mkoani humo wamekuwa kikwazo kikubwa cha kumaliza tatizo la mimba za utotoni, kutokana na kugeuza mimba hizo kama fursa za kujipatia mali, ambapo kesi inapokuwa ikiendelea mahakamani wao huenda kumaliza na upande wa mtuhumiwa, kwa kupewa pesa ama mifugo na kisha kuacha kuhudhulia mahakamani kutoa ushahidi na kesi kufutwa.

“Mimi nilishakutana na kitu kama hiki kuna kesi moja nilikuwa naishughulikia ya mwanafunzi kupewa ujauzito, lakini cha ajabu wazazi wa huyo binti wakakutana na upande wa mtuhumiwa wakamailizana kwa kupeana fedha huku mimi nikiwa sijui, mara nikaanza kukosa ushirikiano kutoka kwao hadi kesi ikafutwa, na mtuhumiwa akachiwa huru,”amesema Makundi na kuongeza;

“Niwaambie tu wazazi mkoani Shinyanga tuache hii tabia ya kugeuza fursa mimba hizi za utotoni kwa malengo ya kujipatia pesa ama mifugo, wanaoumia ni watoto sababu wanazima ndoto zao na kuingia kwenye majukumu ya kiutuuzima ambayo hawayawezi, hivyo naomba tuungane kwa pamoja kutokomeza huu ukatili dhidi ya watoto,”ameongeza.

Habari Kubwa