Waziri aagiza uchunguzi wa  mkataba machinjio Dodoma

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Waziri aagiza uchunguzi wa  mkataba machinjio Dodoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda kamati ya watu watano kupitia upya mkataba wa uendeshaji wa machinjio ya kisasa ya Tanzania Meat Company Dodoma (TMCL) yanayoendeshwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na Kampuni ya Uwekezaji (Nicol).

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

Sababu za kufanyika kwa uchunguzi wa mkataba huo ni kujiridhisha kama umezingatia thamani ya uwekezaji wa pande zote mbili, ikiwamo mgawanyo wa hisa wa asilimia 49 za NARCO na asilimia 51 za Nicol. 

Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ilieleza kuwa Mpina alifikia hatua hiyo juzi baada ya kufanya ziara katika machinjio hayo na kubaini upungufu mkubwa wa kimfumo na kiuendeshaji.

Waziri huyo alikaririwa akisema kuwa timu hiyo ya watalaamu pia itapitia kuona kama pande zote mbili zimetekeleza matakwa ya mkataba wao na sababu zilizoikosesha serikali gawio lake kwa miaka yote nane tangu mradi huo ulipoanza.

Pia Waziri Mpina alikaririwa akisema kuwa masharti ya mkataba huo yanataka kuwepo kwa kipengele cha kufanyika mapitio ya mkataba kila baada ya miaka mitano lakini hadi sasa, licha ya miaka minane kupita, mkataba huo haujawahi kupitiwa na hivyo kukiuka makubaliano.

Aidha, Waziri huyo alishangazwa na kitendo cha machinjio hayo kusubiri wateja wa kuchinjiwa mifugo badala ya kuzalisha na kununua mifugo kwa ajili ya kuchinja kama malengo yaliyokuwapo wakati wa uanzishwaji wa mradi huo. 

Kasoro nyingine alizozibaini Waziri Mpina ni pamoja na migogoro isiyoisha ya kiutawala na pia baadhi ya kampuni kuacha kutumia machinjio hayo kwa visingizio mbalimbali huku pia yakipoteza masharti ya nembo ya ‘halal’.

Kutokana na kasoro hizo, ndipo Waziri Mpina alipounda timu ya watu watano wanaotoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kufanyia tathmini mkataba huo ndani ya siku tano na kuwasilisha taarifa hiyo kabla ya kufanyika kwa kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa machinjio hiyo.

Alisema kamati hiyo ikijiridhisha kuwa mkataba huo hauna masilahi kwa taifa, basi uvunjwe mara moja.

MIFUGO HABA KONGWATaarifa hiyo ilieleza kuwa, wakati alipokuwa katika ranchi ya Kongwa mkoani Dodoma, Waziri Mpina aliagiza uongozi wa ranchi hiyo kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba mwakani, hekta 19,000 ziwe zimeshaandaliwa kwa ajili ya malisho badala ya hekta 3,000 za malisho zilizopo sasa.

Ilielezwa zaidi kuwa, hatua hiyo ya Waziri Mpina ilitokana na taarifa ya meneja wa ranchi hiyo,  Euzebius Rwiza Mtayabaru, iliyoeleza kuwa kati ya eneo la hekta 38,000 zilizopo katika ranchi hiyo, ni hekta 3,000 tu ndizo zilizoendelezwa kwa ajili ya malisho huku eneo la hekta 35,000 likiwa vichaka.

Aidha, Waziri Mpina aliagiza kuwa kufikia Desemba mwakani,  idadi ya ng'ombe katika ranchi hiyo iwe imeongezeka na kufikia walau 20,000, kondoo 5,000 na mbuzi 5,000, badala ya hali iliyopo sasa ya kuwapo kwa idadi ndogo ya mifugo inayotunzwa ambayo ni ng'ombe 8,647, mbuzi 1,438, kondoo 535 na farasi wanane.

Katika hatua nyingine, Mpina aliutaka uongozi wa ranchi hiyo kuweka bei nafuu ya ruzuku ili kuwawezesha wafugaji wadogo kumudu gharama ya kununua mitamba bora kuliko ilivyo sasa ambapo wanunuzi huuziwa ng'ombe hao hadi kufikia Sh. milioni mbili, bei ambayo wafugaji wengi wadogo hawawezi kuimudu. 

Katika taarifa hiyo, Mpina alikaririwa akisema kuwa NARCO inapaswa kubadilisha fikra ili kuwezesha kufikiwa malengo ya kuifanya ranchi hiyo kuwa kitovu cha mafunzo ya ufugaji bora wa kisasa kwa wafugaji wadogo nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Victor Mwita, alimweleza Waziri Mpina kuwa lengo la kuanzishwa ranchi hizo ni kuwawezesha wafugaji wadogo kuuziwa madume bora kwa bei ya ruzuku ili mwishowe waweze kufuga kisasa.

Kaimu Meneja Mkuu wa NARCO, Prof. Philemon Wambura, alimweleza Waziri Mpina kuwa watasimamia kikamilifu maelekezo yake ili kufanikisha azma ya ranchi hiyo kuwa ya mfano na kwa sasa wameanza mpango wa kuwa na hekta 10,000 kwa ajili ya malisho. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, White Zuberi, alimshukuru Waziri Mpina kwa maelekezo yake kwa sababu yatasaidia kuongeza uzalishaji utakaoiwezesha halmashauri kukusanya mapato zaidi yatokanayo na biashara hiyo ya mifugo. 

Habari Kubwa