Waziri aanika sababu foleni mizigo bandarini

04Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri aanika sababu foleni mizigo bandarini

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema mrundikano wa malori ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam unasababishwa na baadhi ya taasisi zinazofanya kazi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambazo hazijaanza kufanya kazi kwa saa 24 kama ilivyoelezwa.

Bandari ya Dar es Salaam.

Tangu Septemba 18, 2017 serikali ilipitisha sheria ya kuzitaka taasisi zote za umma, kufanya kazi kwa saa 24, lakini baadhi hazijadai agizo hilo, hivyo kusababisha kuchelewa kutolewa kwa mizigo.

Kamwelwe aliyaeleza hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wake na wachimbaji wakubwa wa madini duniani na wafanyabiashara waliokutana kwa lengo la kujadili changamoto zinazokwamisha kupitisha mizigo katika bandari hiyo kwa asilimia 100 na kiwango cha utoaji mizigo ni asilimia 25 hadi 40.

“Kumekuwapo na upotoshaji mkubwa kuwa mzani uliopo katika Bandari ya Dar es Salaam unasababisha foleni ya malori kutoka bandarini. Hilo si kweli kwani kuna mizani miwili na zinafanya kazi vizuri bila matatizo yoyote na kwa sekunde 55 yanapimwa malori mawili tena inafanya kazi kwa saa 24,” alisema.

“Kinachosababisha foleni ni changamoto zetu wenyewe watu wa TPA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mamlaka zingine zinazofanya kazi na bandari ambazo zinatakiwa kufanya kazi kwa saa 24 lakini hazifanyi hivyo,” alisema.

Kamwelwe alisema ili kumaliza changamoto hiyo, ameshamwandikia barua Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mipango, ili watumishi wa wizara hiyo wafanye kazi katika bandari hiyo ambayo ina jengo refu linaloweza kutosha watumishi wa idara zote.

Kuhusu mkutano huo, Kamwelwe alisema walikutana na wawakilishi wa zaidi ya kampuni  10 zikiwamo za Bridge Shipping, Acess World, Impala Terminals, Trafigula and Reload Logistics ambazo zinasafirisha madini kwenda nchi mbalimbali duniani, ikiwamo China.

Alisema katika mkutano huo wafanyabiashara hao wamelalamikia mizigo kuchelewa kutoka bandarini, kuwapo kwa sera ambazo hazina uwiano na nchi zingine wanazoshirikiana nazo hasa usawa wa mizigo.

Kamwelwe alisema wameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo ikiwamo  kushirikiana na taasisi zingine kufanya kazi kwa saa 24 katika bandari hiyo na watakutana tena mwezi ujao kujadili kama wameridhishwa na maboresho yanayofanywa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema tangu Jumapili iliyopita, zaidi ya malori 300 yameshapimwa na kupita katika mzani huo hali inayoonyesha mzani si changamoto.

Habari Kubwa