Waziri ahimiza matumizi wataalamu madini

09Nov 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Waziri ahimiza matumizi wataalamu madini

SERIKALI imewaagiza wachimbaji madini kuwatumia wataalamu kutoka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kupima maeneo ya miamba ya migodi kabla ya kuanza kuchimba badala ya kutumia ushirikina.

Aidha, serikali imesema imejipanga kutoa elimu ya uchimbaji madini, uchenjuaji na ujasiriamali kwa wachimbaji wadogo ili kuwapa namna ya kuhifadhi fedha zitokanazo na madini.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanislaus Nyongo, katika mdahalo wa uziduaji sekta hiyo unaoendelea jijini hapa katika maadhimisho ya wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki).

Nyongo alisema serikali imeamua kutoa wataalamu hao ili kuwasaidia wachimbaji kupata elimu kutokana na wengi wao kukosa maarifa juu ya uchimbaji na badala yake hutumia imani za kishirikiana katika uchimbaji jambo linasababisha kutumia nguvu nyingi bila mafanikio.

"Unakuta mchimbaji akifika mgodini anaweka mate mkononi halafu anayapiga kwa mikono miwili yanaporukia ndiyo anaenda kuchimba anadai mwamba uko upande huo," alisema Nyongo.

Kutokana na hilo alisema hivi sasa wanatoa wataalamu kwa wachimbaji ambao wanakwenda kuwapimia kwenye miamba kabla ya kuchimba na kuwaelekeza wapi madini yapo.

Nyongo pia alisema mchimbaji anakwenda kuuza nyumba, mwingine ng'ombe na kupeleka fedha migodini lakini anajikuta fedha yote imepotea na kufisilika kutokana na kutumia imani za kishirikina badala ya elimu ya kitaalamu kutoka Stamico.

"Kwa upande wa wachimbaji wakubwa haina shida, kazi iko kwa wachimbaji wadogo," alisema Nyongo.

Akizungumzia elimu ya ujasiriamali kwa wachimbaji, alisema ni suala muhimu sana kwa sababu wengi wao wamekuwa wakitumia fedha wanazozipata katika madini badala ya kuhifadhi kwa ajili ya kufanyia maendeleo.

"Tunaendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wachimbaji ili wahifadhi fedha hata pale wanapokosa madini wanakuwa na akiba," alisema Nyongo.

Kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika uchimbaji madini, aliwataka kutoa ushirikiano wakati wa ukaguzi, huku akiwasisitiza wanawake kuacha kukubali kutumika kwa miili yao kubeba madini kwa kuficha kutoka machimboni.

"Naomba niseme watu msikubali kuficha madini mpaka sehemu zisizo faa mfano madini ya Tanzanite katika mashine za kuscan hayatoi sauti hivyo wakijua unayo lazima wakukague," alisema Nyongo.

Habari Kubwa