Waziri aipongeza NMB elimu kwa wakulima

06Aug 2020
Happy Severine
Bariadi
Nipashe
Waziri aipongeza NMB elimu kwa wakulima

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Inoccent Bashungwa, ameipongeza benki ya NMB kwa utoaji wa elimu ya kifedha bure kwa wajasiriamali mbalimbali wakiwamo wakulima, wavuvi na wafugaji kwenye maonyesho ya Nanenane kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mjini hapa.

Amesema jambo ambalo linalofanywa na benki hiyo ni muhimu sana hasa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji ambao wana uhitaji mkubwa wa elimu ya usimamizi wa fedha.

Bashungwa alisema hayo jana baada ya kutembelea banda la benki hiyo na kufurahishwa kukuta wakulima, wafugaji na wavuvi wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo.

Alisema lengo kubwa la serikali kuanzisha maonyesho hayo ni kutaka wananchi walioko kwenye sekta ya kilimo kupata teknolojia za kuwawezesha kuongeza tija kwenye uzalishaji wao na mikopo.

“Wamekuwa wakipata hizi teknolojia, lakini bado tatizo lipo kwenye kujua wapi wapate mikopo, lakini jinsi ya kusimamia pesa zao. Nimefurahishwa sana kuona hili NMB mnalitekeleza kwa ufanisi hapa Nanenane,” alisema Bashungwa.

Hata hivyo, waziri huyo aliiomba benki hiyo kutoa elimu kama hiyo kwenye vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) ambavyo vimekuwa na matatizo ya ubadhirifu wa fedha za wanachama.

“Niwaombe NMB kuisaidia serikali kutoa elimu hii kwa AMCOS, baadhi yake bado zina matatizo kwenye usimamizi wa fedha. Ingawa serikali tumeendelea kupambana nalo, elimu hii ni muhimu sana kwao,” alisema Bashungwa.

Alisema elimu ambayo inatolewa na NMB kwenye maonyesho hayo, ni sehemu ya malengo ya serikali ya kuwainua kiuchumi wakulima, wavuvi na wafugaji ikiwa pamoja na kuzalisha kwa tija.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse, alisema benki hiyo imetoa Sh. bilioni 161 kwenye mazao ya tumbaku, kahawa na pamba.

Magesse alisema fedha hizo zimepelekwa kwenye mazao hayo kama mkopo na wanufaika wakuu ni wakulima kupitia takribani AMCOS 700.

Habari Kubwa