Waziri akunwa kazi za SAGCOT

14Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri akunwa kazi za SAGCOT

NAIBU Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, amepongeza kazi inayofanywa na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT), kwa kuwafikia wakulima wengi katika ukanda huo na kufanya mageuzi kwenye sekta ya kilimo kwa kuongeza tija katika uzalishaji.

NAIBU Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa picha mtandao

Akizungumza katika ziara yake ya kwanza  alipotembelea  kituo hicho jijini Dar es Salaam  mwishoni mwa wiki ili kujionea utendaji kazi wake, Bashungwa alisema amefurahishwa na kazi zinazofanywa na  kituo hicho ikiwamo kuwaunganisha wakulima na kuwajengea uwezo na mbinu za kilimo biashara.

“Ziara yangu katika ofisi yenu imetokana na kuona kazi nzuri na ushuhuda mbalimbali kutoka kwa wakulima katika mikoa ya Njombe na Iringa, hivyo ikanisukuma  niwatembelee  ili tufahamiane na kujifunza kazi zenu,” alisema Bashungwa.

Alisema utendaji kazi wa SAGCOT umeleta matokeo chanya kwa wakulima katika mikoa ya nyanda za juu kusini, hivyo ni muhimu kwa wadau mbalimbali wa kilimo kote nchini kujifunza kupitia mfumo unaotumiwa na SAGCOT, ili  kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.

Alisema  kwa kufuata mfumo huu wa SAGCOT,  utekelezaji wa Mpango wa awamu ya  Pili wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP  II) utakuwa wa mafanikio, kwa kuwa njia nzuri imeonyeshwa kupitia maeneo ambayo SAGCOT inafanya kazi zake.

“Wakulima wa chai mkoani Njombe wamefaidia kwa kilimo cha chai kupitia washirika wa SAGCOT ambao ni kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe (NOSC), hii inaonyesha ni kwa namna gani SAGCOT imejipanga kuleta mapinduzi ya kilimo nchini,” alisema Bashungwa.

Aidha, aliagiza NOSC kueneza utaalamu wa kuendeleza zao la chai katika mikoa mingine ili kuliendeleza kwa sababu ardhi nzuri ya kilimo cha zao hilo iko katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hivyo ni jukumu la wadau katika kuendeleza.

Alisema kwa kushirikiana kwa pamoja tutaweza kutekeleza ASDP II kwa muda uliopangwa na pia kufanya azima ya serikali ya kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025 kufikiwa kwa vitendo kwa kuwa njia ya kuelekea katika mafanikio imeshaanza kupitia SAGCOT.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, alishukuru ujio wa naibu waziri huyo na taarifa ya utendaji kazi wa kituo  na mipango ya kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo nchini kwa kuanza na ukanda wa nyanda za juu kusini.

“Ujio wa mheshimiwa naibu waziri umekuwa  ni faraja kwetu kwa sababu ameweza kufahamu dhumuni la kituo chetu na zaidi ametoa mapendekezo na maagizo ambayo kama SAGCOT tumeyapokea na tutakwenda kuyatekeleza kikamilifu,” alisema Kirenga.

Alisema mapendekezo yake yote yatafanyiwa  kazi lengo likiwa kuboresha huduma katika kukuza na kuendeleza kilimo nchini kwa kumwinua mkulima mdogo kwa kushirikana na wadau na watoa huduma mbalimbali za kilimo.

Habari Kubwa