Waziri atafutia ufumbuzi mkwamo malori

14May 2022
Benny Mwaipaja
Nipashe
Waziri atafutia ufumbuzi mkwamo malori

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema serikali itawasiliana na Mamlaka za Kenya ili kutatua changamoto ya malori ya mizigo yanayovuka kupeleka bidhaa nchini humo kutumia muda mrefu kupata vibali vya kuvuka mpaka wa Horohoro.

 

Dk. Nchemba alisema hayo baada ya kuzungumza na madereva wa malori yanayobeba mizigo kwenda Kenya katika mpaka wa Horohoro, akiwa njiani kwenda Mombasa nchini Kenya kwenye mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Madereva hao walisema wanapata usumbufu mkubwa kwa sababu wanatumia takriban siku 14 hadi 21 kuvuka mpaka wa Horohoro kwenda Kenya, wakati madereva wa Kenya wanaoingia Tanzania wanatumia siku tatu kuvuka mpaka huo.

Walisema kuchelewa kuvuka mpaka kunawaletea matatizo makubwa ikiwamo kutumia gharama kubwa zisizolingana na posho za safari wanazopewa na waajiri wao, lakini pia kuna baadhi ya bidhaa zinaharibika kabla ya kuvuka mpaka.

Dk. Nchemba alisema amebaini kuwa ucheleshwaji wa huduma ya forodha kwa Kenya unatokana na nchi hiyo kutoanza kutumia Mfumo wa Pamoja wa Huduma ya Forodha kama walivyokubaliana.

Alisema kuwa magari ya Kenya hayapati changamoto hiyo ya foleni kwa kuwa tayari Tanzania wanatumia mfumo huo na mizigo yote ya Kenya hupata vibali kabla ya kufika katika mpaka na malori kupita bila tatizo.

Dk. Nchemba alisema atawasiliana na waziri mwenzake wa fedha wa Kenya ili kuanza kutekeleza makubaliano ya kuweka mfumo huo wa pamoja na forodha kwa kuwapeleka watumishi wa nchi hiyo upande wa Tanzania ili kuharakisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwaondolea adha wafanyabiashara na madereva wanaotumia mpaka huo kufanya biashara zao.

Habari Kubwa