Waziri ataka kilimo kipya

03Aug 2017
Na Waandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
Waziri ataka kilimo kipya

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, amewahimiza viongozi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi vijiji kuhakikisha wanasimamia uwapo wa bei nzuri ya mazao kulingana na bei katika soko la Dunia ili kukifanya kilimo kuwa na tija na kufikia azma ya maendeleo ya viwanda nchini.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.

Prof. Maghembe aliyasema hayo jana kwenye ufunguzi wa Maonyesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na sherehe za Nanenane Kanda ya Mashariki kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini hapa.

  “Ili Serikali na nchi kwa ujumla iweze kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ikiwamo kuimarisha maendeleo ya viwanda, suala la masoko la uhakika la mazao halinabudi kuzingatiwa kufuatia asilimia 90 ya mazao kutegemewa katika viwanda kama malighafi,” alisema Prof. Maghembe.

  Alisema ni muhimu soko la mazao lianzishwe mara moja ili kuondoa bei holela za mazao sambamba na kusimamia ubora wa vifungashio na kuondoa masuala ya rumbesa.

  “Hatuwezi kufikia taifa la kati huku tukiwa tumebeba wakulima zaidi ya milioni 33 bila kuwa na bei stahiki ya mazao, huku ukitaka kuwa na uchumi wa kati,” alisema Prof. Maghembe.  

Aliwataka wakulima kusimamia na kufuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo kwa kufuata misingi ya sayansi katika kilimo na baadaye wataona manufaa ya kilimo.  

  Aliwahimiza kuwa miaka nane iliyobaki kutimiza malengo ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025 kuhakikisha wanatumia mazao ya mbegu za GMO ili kuongeza uzalishaji wa mazao.

  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, aliwataka waliouziwa viwanja na kukodishwa kwa ajili ya shughuli tofauti na maonyesho katika uwanja huo kuondoka wenyewe mapema kabla hawajapewa notisi ya miezi mitatu kupisha maonyesho hayo.  

Dk. Kebwe alisema Chama cha Wakulima (TASO) kiliamua kuwakodisha watu kwa ajili ya makazi na biashara tofauti na makusudio ya maonyesho, jambo ambalo halileti maana ya maonyesho na kwamba vikao vya kamati kupitia Tamisemi wameamua kutoa notisi kwa wakazi hao ili wapishe maeneo hayo.

  Alisema uwanja huo ulitengwa mahususi kwa ajili ya maonyesho ya kilimo, uvuvi na mifugo na kwamba kufanya shughuli nyingine tofauti hakutawezesha nia ya elimu iliyokusudiwa kuwafikia wakulima.

  Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Cliford Tandari, alisema baada ya maonyesho hayo kurudishwa katika usimamizi wa Tamisemi, wameongeza makusanyo hadi Sh. milioni 80 na wanaweza kufikia Sh. milioni 140 baada ya maonyesho kumalizika na fedha hizo zinatawasaidia kutatua changamoto katika uwanja huo ikiwamo uchache wa maji, ukosefu wa uzio na kuboresha uwanja kuwa na maonyesho ya kudumu.

*Imeandikwa na Christina Haule na Idda Mushi

Habari Kubwa