Waziri ataka NHC kuwekeza miradi mkakati

25Nov 2021
Munir Shemweta
Missenyi
Nipashe
Waziri ataka NHC kuwekeza miradi mkakati

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuendelea kuwekeza miradi ya kimkakati itakayoliwezesha kujiongezea kipato.

Dk. Mabula alisema hayo juzi wakati akikagua mradi wa jengo la kibiashara la NHC lililiko mpakani mwa Tanzania na Uganda, Mutukula, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.

Mabula ambaye alikuwa katika  ziara ya siku mbili mkoani Kagera, ilichofanya NHC kujenga jengo la kibiashara katika mpaka huo, ndicho serikali inachokitaka pale inapokuwa na taasisi zinazojitegemea katika uendeshaji pia ziwe na njia tofauti za kujiongezea kipato kitakachosaidia kuongeza miradi mingine. 

Kwa mujibu wa Dk. Mabuka, mradi wa jengo la biashara Mutukula unatoa fursa kwa wafanyabiashra kutoka nchi jirani ya Uganda kuja Tanzania kununua bidhaa kwa kuwa awali ilikuwa aibu kuona wafanyabiashara wakienda kununua bidhaa katika maduka ya nchi hiyo.

"Ilikuwa aibu tunaenda upande wa pili kununua bidhaa, lakini sasa na wao waje hapa kufanya biashara na hii ni alama tosha kuwa tunaanza kubadilika," alisema Naibu Waziri.

Dk. Mabula aliongeza kuwa ana imani mradi huo ukienda vizuri, eneo lingine linalokusudiwa kujenga maduka, litapata msaada wa fedha za ndani zitakazopatikana kupitia mradi huo.

Aliongeza kuwa ni kweli wafanyabiashara wadogo, maarufu kama machinga, hawawezi kupanga katika jengo la mradi huo, lakini shirika linaweza kujenga maduka kuzunguka jengo hilo yanayoweza kubadilisha sura ya eneo kuonyesha kuwa limepangwa na visiwe viduka visivyoonyesha tofauti kati ya eneo lililopangwa na lisilopangwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Projestus Tegamaisho, aliishukuru NHC kwa uamuzi wake wa kuwekeza mradi huo katika eneo la Mutukula. Aliiomba NHC kuangalia uwezekano wa kuwekeza mradi kama huo katika mji unaopanuka wa Bunazi wilayani Missenyi.

Meneja wa NHC Mkoa wa Kagera, Maneno Mahenge, alisema mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 99 na umetumia asilimia 50 tu ya eneo lake lenye ukubwa wa mita za mraba 7,900.

Habari Kubwa