Waziri atembelea kiwanda bila kukuta wafanyakazi

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Tabora
Nipashe
Waziri atembelea kiwanda bila kukuta wafanyakazi

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amefanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha nyuzi Tabotex mkoani Tabora na kukuta hakina wafanyakazi.

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, picha mtandao

Wafanyakazi hao walimkimbia msimamizi wa kiwanda hicho, na kumsababisha ashtuke mbele ya Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

Video fupi inayoonyesha namna msimamizi wa kiwanda hicho, alivyoshtuka baada ya kujikuta yupo peke yake, mbele ya viongozi hao, ilianza kusambaa juzi kwenye mitandao ya kijamii.

Katika ziara hiyo, Bashe alikuta uzalishaji duni wa nyuzi tani 6,200 kwa mwaka, tofauti na malengo ya kiwanda hicho, huku mwekezaje naye akisuasua katika uendeshaji.

Bashe alilazimika kuanza kumuhoji msimamizi wa kiwanda hicho, ambaye alianza kujiuma uma huku akiwa hana uhakika na kile anachokijibu.

“Kwa mwaka tunazalisha tani 6,200 za uzi na ‘input’ (pembejeo) tani 100 hadi 200 kwa mwezi,” alijibu huku akitafuta wenzake wamsaidie.

“Niko peke yangu hapa…. kumbe wenzangu wamenikimbia.”

Alipoulizwa kama kuna wafanyakazi alisema wapo 180 na wanapokezana kuingia kazini watu 60 kwa zamu tatu.

Alisema pia wanafanya mazungumzo na wawekezaji wa sekta binafsi kwa ajili ya kushirikiana na kiwanda hicho katika uzalishaji.
Alipoulizwa sababu za kutozalisha licha ya kuwapo kwa miundombinu na pembejeo kupatikana, hakuwa na jibu.

Naye Mwanri alisema miaka minne iliyopita, mwekezaji huo alishaahidi kumtafuta mwekezaji raia wa China ambaye atawekeza Dola za Marekani milioni 500.

Alisema alishaomba reli ijengwe kufika eneo hilo la kiwanda kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho.

Habari Kubwa